Vurugu bungeni Uingereza kwa maazimio ya Gaza
22 Februari 2024Wabunge hao walikuwa wakijadiliana maazimio matatu tafauti lakini yote yanayohusiana na vita hivyo.
Hata hivyo, maazimio yote hayo ya siku ya Jumatano (Februari 21) yalikuwa ya kisiasa zaidi kuliko ya kimaamuzi, kwani serikali haina ulazima wa kuyatekeleza.
Mjadala uligeuka vurugu, baada ya wabunge wa chama kinachotawala, Conservative, na wa chama cha upinzani cha Scottish National Party (SNP) kumshutumu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Lindsay Hoyle, kwa kuukiuka utaratibu wa kibunge.
Soma zaidi: Israel inapaswa kutafakari kabla ya kuchukua hatua, Rafah
Zogo hasa lilizuka kwenye hoja ya mbunge wa SNP iliyotaka usitishwaji wa haraka wa mapigano, kuachiliwa kwa mateka wote wa Kiisraeli wanaoshikiliwa naHamasna kukomeshwa kwa "adhabu ya jumla jamala wanayoadhibiwa Wapalestina" kutokana na kampeni ya kijeshi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Lakini chama kikuu cha upinzani, Labour, kiliwasilisha aina nyengine ya hoja hiyo, inayotaka kusitishwa mapigano kwa sababu za kibiinadamu, bila kutaja adhabu ya jumla jamala.
Conservative yataka kwanza Hamas iwaachie mateka
Kwa upande wake, Conservative ilikuja na marekebisho yake yenyewe yanayounga mkono usitishwaji haraka wa mapigano kwa misingi ya kibinaadamu, utakaofuatiwa na usitishwaji wa kudumu na endelevu.
Conservative inasema usitishwaji halisi wa mapigano unaweza tu kutokea endapo kundi la Hamas litawaachia huru mateka wote na pia kuachia madaraka ya kuitawalaGaza.
Pale Spika Hoyle aliporuhusu kura kupigwa kwenye maazimio yote matatu, wabunge wa Conservative walikasirika wakisema uamuzi huo ulikuwa kinyume na taratibu za kibunge na kumshutumu spika huyo kwa kuwapendelea wapinzani, shutuma alizozikanusha.
Soma zaidi: Shirika la mpango wa chakula duniani WFP lasitisha ugawaji chakula kaskazini mwa Gaza
"Mimi ni mtiifu kwa Bunge hili. Mimi ni mkweli kwa Bunge hili. Nina imani kwa wajumbe wote. Nimejaribu kufanya kile nilichodhani ni sahihi kwa pande zote. Ni jambo la kusikitisha na naomba radhi kwa uamuzi ambao haukwenda kama nilivyotarajia. Sasa nasema, nitakutana na viongozi wote na wanadhimu na kujadiliana nao kile kilicho bora zaidi kuweza kusonga mbele." Alisema spika huyo, ambaye alipata ubunge kupitia chama cha upinzani cha Labour.
Vurugu hii ya kisiasa ni ishara ya jinsi mzozo huu wa Mashariki ya Kati ulivyowagawa wanasiasa na raia wa Uingereza.
Wabunge wengi wa Conservative na SNP walitoka nje, na kuwapa nafasi wenzao wa Labour kupitisha azimio la kusitisha mapigano bila kura rasmi iliyokamilika.
Reuters