1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama ndugu vya CDU CSU vyakabwa na mzozo wa wahamiaji

Oumilkheir Hamidou
1 Julai 2018

Viongozi wa vyama ndugu vya kihafidhina Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union-CSU wanatahadharisha dhidi ya hatari ya kuzuka mfarakano kati yao kuhusiana na mzozo wa wahamiaji.

https://p.dw.com/p/30cqd
Deutschland | Merkel trifft Seehofer im Kanzleramt
Picha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

Kabla ya vikao vya dharura vya uongozi wa vyama vya CDU na CSU, leo jioni na usiku, wanasiasa wa vyama hivyo ndugu waneonya dhidi ya mfarakano kati ya vyama hivyo ndugu. Waziri wa zamani wa utamaduni Hans Meier wa chama cha CSU ameliambia gazeti la "Frankfurter Allgemeine" toleo la jumapili, anataraji " kwa mara nyengine tena busara itaibuka na ushindi.""Malumbano na mfarakano havitawatanabahisha wapiga kura" amesema na kutahadharisha dhidi ya kitisho cha kuvurugika mfumo wa vyama vya kisiasa nchini.

Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer (kushoto) na mwenyekiti wa kundi la wabunge wa CSU Alexander Dobrindt
Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer (kushoto) na mwenyekiti wa kundi la wabunge wa CSU Alexander DobrindtPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Mfarakano utadhoofisha nafasi ya ushindi vya vyama ndugu vya CDU/CSU

"Kuvunjika umoja wa wahafidhina kutadhoofisha nafasi ya kushinda uchaguzi vyama vya umma " amesema pia mwenyekiti wa tawi la CDU katika jimbo la Thüringen Mike Mohring."Hali hiyo inaweza pia kuathiri matokeo ya uchaguzi katika majimbo ya Hesse, Sachsen naa Brandenburg pia amesisitiza.

Jana usiku, kansela Angela Merkel na waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer walikutana katika kikao cha dharura katika ofisi ya kansela mjini Berlin kujaribu kusaka njia za kuufumbua mzozo unaotishia umoja wao. Matokeo ya mkutano huo hayajulikani.

Mzozo uliopo umesababishwa zaidi na madai ya chama cha CSU ,  kutaka wakimbizi ambao tayari wamesajiliwa katika nchi nyengine za Umoja wa ulaya wahamishwe haraka toka mpaka wa Ujerumani.

Kansela Merkel anapinga hatua za upande mmoja katika suala hilo na anapigania maridhiano miongoni mwa nchi za umoja wa Ulaya. Na kusema kweli amefanikiwa kansela Merkel katika mkutano wa kilele wa umoja wa ulaya, alkhamisi na ijumaa iliyopita mjini Brussels kufikia maridhiano pamoja na viongozi wenzake tofauti kuhusu suala hilo.

Wakimbizi wanaosubiri kusajiliwa
Wakimbizi wanaosubiri kusajiliwaPicha: picture-alliance/dpa/M. Elhorsy

Maridhiano yaliyofikiwa ndani ya Umoja wa Ulaya yanatiliwa shaka

Mkuu wa kundi la wabunge wa chama cha CSU katika bunge la shirikisho Bundestag, Alexander Dobrindt anatilia shaka maridhiano hayo. Akizungumza na gazeti la Bild" toleo la leo jumapili, Alexander Dobrindt anasema "ana wasi wasi kama makubaliano yote ya Umoja wa ulaya yatatekelezwa." Anazitaja hoja kinzani zinazotolewa katika baadhi ya mataifa wanachama.

Hata hivyo msaidizi wa waziri mkuu wa jimbo la kusini la Bavaria, Ilse Aigner amekitolea wito chama chake kiregeze kamba. Anasema vifungu kadhaa muhimu vimetajwa katika makubaliano yaliyofikiwa Brussels..

Leo jioni na pia usiku, viongozi wa CDU na wale wa CSU watakutana mijini Berlin na Munich pia.CSU wanabdi wataamke kama makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Umoja wa ulaya kuhusu wahamiaji yamewaridhisha au la.Kansela Merkel anatilia mkazo umuhimu wakkuendelezwa umoja wao.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/epd/AFP

Mhariri: Caro Robi