Vyama vya siasa Mali vyaruhusiwa kuendesha shughuli zake
11 Julai 2024Taarifa iliyotolewa jana na baraza la mawaziri ambalo idadi yake kubwa ni viongozi wa kijeshi iliieleza kuwa serikali imeamua kuondoa marufuku ya vyama vya siasa na shughuli za vyama hivyo.
Kiongozi wa serikali ya kijeshi ya Mali, Kanali Assimi Goita alihalalisha marufuku hiyo kwa kuelezea kuwepo kwa mijadala isiyo ya msingi ya vyama vya siasa na upotoshaji ambayo alisema ilihatarisha mazungumzo ya kitaifa yanayoendelea kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Mali.
Kwa wakati huo vyama vya siasa vilikuwa vinapinga uamuzi wa Kanali Goita wa kubakia madarakani baada ya muda uliowekwa wa Machi 2024 kumalizika, wakitaka kurejea kwa utawala wa kiraia.
Soma pia:Utawala wa jeshi nchini Mali wanuia kurejesha shughuli za siasa ilizozizuia tangu Aprili
Vyama vikuu na vilivyobaki vya upinzani vilisusia "mazungumzo", ambayo yaliendelea na wafuasi wa serikali, ambao mnamo Mei walitoa "mapendekezo" kwamba wanajeshi wabaki madarakani "kwa miaka miwili hadi mitano ya ziada."
Mapendekezo hayo pia yalilenga kumruhusu mkuu wa sasa wa serikali kuu aruhusiwe kugombea katika uchaguzi wowote ujao wa urais.