Vyama vya upinzani kushiriki katika uchaguzi wa rais nchini Nigeria hapo kesho
20 Aprili 2007Vyama vikuu vya upinzani nchini Nigeria vimesema kuwa vitashiriki katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika kesho nchini humo hapo kesho.
Hadi muda mfupi uliopita vyama hivyo vilitishia kususia uchaguzi huo na kutaka uahirishwe.
Lakini katika dakika ya mwisho vimeamua kuwa vitashiriki lakini kila chama kitasimama peke yake tofauti na wazo la hapo awali juu ya kusimama pamoja na kumkabili mjumbe wa chama kinachotawala.
Lakini kufuatia ushindi wa chama kinachotawala katika uchaguzi wa majimbo mwishini mwa wiki kila ishara inaonesha kuwa mjumbe wa chama hicho ndie atakeibuka kuwa mshindi kesho yaani bwana Umaru Yaradua wa chama cha People’s Democratic Party.
Chama hicho kilishinda katika majimbo 27 kati ya yote 34.
Katika mstari wa mbele kumkabili mjumbe wa chama kinachotawala ni wagombea wa vyama vya Action Congress na Nigeria People’s Party—bwana Atiku Abubakar na Muhammadu Buhari.
Wagombea wengine wanatoka katika vyama vingine 21.
Wakati huo huo huku kukiwa na mvutano, rais Oleseguni Obasanj ametoa mwito juu ya kuchua hatua za kuepusha udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi wa kesho.
Jumuiya ya kimataifa imetoa mwito kwa viongozi wa Nigerian kuwataka waepushe vurumai na matendo ya utumiaji nguvu.
Akiwahutubia wananchi wake kwa njia ya radio rais Obasanjo amesema leo kuwa macho ya dunia nzima yanaangaza nchini Nigeria . Bwana Obasanjo amewata wananchi wake watumie fursa ya uchaguzi wa kesho kulinda heshima yao na kutimiliza matumaini ya marafiki wa Nigeria duniani kote.
Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na asasi za kiraia zimeeleza wasiwasi juu ya uchaguzi wa kesho iwapo kweli utafanyika kwa haki na katika mazingira huru.
Mashirika hayo yamesema kuwa tume ya uchaguzi pamoja na serikali hazijasaidia sana katika utekelezaji wa sera za uwazi juu ya uchaguzi huo.
Ikiwa mambo yataenda salama, uchaguzi wa kesho utakuwa wa kwanza nchini Nigeria tokea mwaka 1960 ambapo serikali ya kiraia itakabidhi madaraka kwa serikali nyingine ya kiraia.
Hatahivyo rais Obasanjo amekiri kwamba palikuwapo hitilafu katika uchaguzi wa majimbo mwishoni mwa wiki jana. Ametoa mwito juu ya kuimarisha taratibu za kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.
ABDU MTULLYA