Vyama vya wafanyakazi vyatangaza mgomo Uturuki
17 Juni 2013Vyama viwili vya wafanyakazi vya Uturuki vimeanza mgomo huo wa nchi nzima kupinga vitendo vya ukandamizaji wa serikali ya taifa hilo dhidi ya waandamanaji, ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Uturuki, Receip Erdogan kujitokeza hadharani na kutetea uamuzi wake wa kuwatawanya waandamanji katika bustani ya Gezi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Muammer Guler amelaani mgomo huo kwa kusema sio halali na kuwaonya waandamanaji kutojitokeza mitaani. Na kwa upande wa polisi wa kutuliza ghasia leo hii pia wameripotiwa kuendelea kufyatua mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kwa lengo la kuwatawanya waandamanaji katika mitaa ya Istanbul na mji mkuu wa Ankara.
Waandamanaji watiwa mbaroni
Duru tofauti kutoka Ankara na Istanbul zinaeleza kuwa karibu watu 600 wamekamatwa katika operesheni ya polisi iliyofanywa jana peke yake.
Vyama vya wafanyakazi KESK na DSK, ambavyo vyote kwa pamoja vinawawakilisha maelfu ya wafanyakazi vimeitisha mgomo wa siku moja wenye lengo la kupinga vitendo vya polisi na kuongeza kuwa vimepanga kufanya maandamano baadae jioni.
Akizungumza na shirika la habari la AFP msemaji wa KESK, Baki Cinar amesema matakwa yao ni kwamba polisi isimamishe mara moja na kuongeza kuwa maandamano hayo yatajumisha wahandisi, madaktari na madaktari wa meno.
Kutawanywa kwa waandamanaji
Awali Jumamosi, polisi wa kutuliza ghasia nchini humo uliisafisha bustani ya Gezi, mjini Istanbul, eneo ambalo wanaharakati walikusanyika kwa takribani kwa siku 18 , mkusanyiko ambao chanzo chake kilikuwa, maandamano ya wanamazingira yaliokuwa na lengo la kupinga jitihada za serikali kukata miti katika eneo hilo la bustani na kujenga jengo la maduka makubwa ya kibiashara.
Lakini baadae maandamano hayo yakaenea nchi nzima, na Uwanja wa Taksim ukawa ndo kitovu cha maandamano. Leo polisi wa kutuliza ghasia wameendelea kuuzingira uwanja huo kwa lengo kwa lengo la kudhibiti kutokea kwa aina yeyote ya mkusanyiko. Hata hivyo jana maelfu ya waandamanaji walijaribu kukusanyika katika eneo hilo lakini polisi hao wa kutuliza ghasia waliwarudisha nyuma kwa kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.
Katika mkutano uliohudhuriwa na zaidi ya wanachama 100,000, kutoka chama chake cha Haki na Maendeleo (AKP) hapo jana, waziri mkuu wa Uturuki Receip Tayyip Erdogan alisisitiza kuwa ni wajibu wake kuamuru polisi kuwatawanya waandamanaji katika bustani ya Gezi kama onyo lake halikuzingatiwa.
Kutokana na hali hiyo ya kutumika nguvu dhidi ya maandamano ya amani Marekani na washirika wake wa nchi za magharibi, sambamba na makundi ya haki za binaadamu wamemkosoa Erdogan kwa namna anavyoushughulikia mgogoro huo.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri:Moahammed Abdul-Rahman