Vyama vyaanza mchakato wa kuunda serikali Ujerumani
28 Septemba 2021Haya yanafanyika wakati ambapo kiongozi wa SPD Olaf Scholz amesema kuwa kama mshindi wa uchaguzi, chama chake tu ndicho chenye idhini ya kuunda serikali.
Wawakilishi kutoka chama cha Kijani na FDP wanatarajiwa kukutana Jumanne kujaribu kutafuta mwafaka kuhusiana na mitazamo yao tofauti kuhusiana na mwelekeo wa Ujerumani. Vyama hivyo ambavyo vinatofautiana katika mambo mengi vimesema mazungumzo haya ni muhimu kabla kwenda hatua inayofuata.
Vyama vya SPD na CDU havitaki washirika wale wale katika serikali ya muungano
Christian Lindner ni kiongozi wa chama cha FDP.
"Tukizungumzia vyama vya kidemokrasia vinavyoweza kufanya mazungumzo ya kuunda serikali, tofauti kubwa mno zinapatikana katika vyama vya Kijani na FDP. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kutafuta maelewano ukizingatia hizo tofauti kubwa zilizopo. Wakati huo huo chama cha Kijani na FDP ndivyo vyama ambavyo vinapinga pakubwa serikali ya muungano jinsi ilivyo kwa sasa," alisema Lindner.
Kwa kuwa vyama vikuu vya SPD na CDU vyote havitaki kuunda serikali mpya na washirika wake waliopita wa serikali ya muungano, vyama vya Kijani na FDP ndivyo vinavyoonekana kuwa muhimu sana katika mazungumzo haya.
Kiongozi wa SPD Olaf Scholz ambaye ni naibu kansela anayeondoka madarakani amesema anataka kuunda serikali mpya kabla Krismasi ikiwezekana. Uundaji wa serikali nchini Ujerumani ni mchakati ambao kawaida unaweza kuchukua wiki kadhaa au hata miezi kutokana na kuwa vyama husika vinazungumzia kwa kina mipango ya serikali mpya ya muungano.
Chama cha SPD ambacho kilipata ushindi mfinyu katika uchaguzi wa Jumapili kimesema leo kwamba kinatarajia kufanya mazungumzo na FDP na chama cha Kijani baadae wiki hii kuhusiana na kuunda serikali ya muungano. Kauli hii ya SPD inaonekana ni mbinu ya kukizuia chama cha Christian Democratic Union CDU kisianze mazungumzo hayo ya kuunda serikali.
SPD kilishinda uchaguzi kwa asilimia 25.7 ya kura
Katika uchaguzi uliopita wa Ujerumani mwaka 2017, mazungumzo ya kuunda serikali yalidumu kwa kipindi cha miezi sita. Wakati huo chama cha SPD kilionekana kuwa tayari kuchukua muda katika suala hilo huku kiongozi wake Olaf Scholz akisema uwezekano wa kuunda serikali kabla Krismasi ni jambo lisilowezekana kabisa.
Chama cha SPD ambacho ndicho chama cha zamani zaidi nchini Ujerumani kilishinda uchaguzi kwa asilimia 25.7 ya kura hiyo ikiwa kimeongeza asilimia 5 ya kura kilizopata katika uchaguzi wa mwaka 2017. Chama cha Kihafidhina na chama chake ndugu cha CSU vilichukua nafasi ya pili kwa kupata asilimia 24.1.
Vyanzo:Reuters/AP/ https://bit.ly/3og8xSe