Vyanzo: Mashambulizi ya Israel yawaua zaidi ya watu 20 Gaza
5 Januari 2025Ofisi inayosimamia usalama wa umma kwenye ukanda huo wa Wapalestina umesema makombora yaliyofyetuliwa na ndege za Israel yamesababisha vifo vya watu 23, huku jeshi la Israel likisema limeyalenga zaidi ya maeneo "100 ya magaidi" katika muda wa siku mbili zilizopita.
Shirika la habari la AFP likimnukuu msemaji wa ofisi hiyo ya ulinzi wa raia Mahmud Bassal, limeripoti kwamba watu 11 waliuawa kwenye nyumba moja kwenye kitongoji cha Sheikh Radwan kaskazini mwa Gaza.
Afisa huyo pia ameongeza kusema kwamba waliouawa ni pamoja na wanawake na watoto.
"Waokoaji bado wanawatafuta watu watano walionaswa kwenye vifusi chini ya nyumba iliyoporomoka," amesema Bassal.
"Waokoaji wanatumia mikono kufukua vifusi kutokana na ukosefu wa vifaa."
Bassal amevituhumu vikosi vya Israel kwa kufanya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya watu kwenye majengo yanayotumika kuwahifadhi, "kwa madai ya kuwalenga wanamgambo".
Mashambulizi hayo ya leo, yanafanya jumla ya idadi ya watu waliuawa mwishoni mwa juma hili kufikia 102. Takwimu hizo ikiwa ni kwa mujibu wa madaktari wa Kipalestina.
Katika shambulizi jingine, watu watano waliuawa kwenye nyumba moja ya familia ya Abu Jarbou iliyopo kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katika mwa Gaza. Hayo pia yameelezwa na ofisi ya ulinzi wa raia ya ukanda huo.
Kulifanywa pia shambulizi jingine huko Khan Younis lililokilenga kituo cha polisi na kuwaua watu watano. Haikuwa wazi juu ya iwapo wote waliopoteza maisha walikuwa polisi ama la.
Israel yajitetea ikisema imewaua wanamgambo kadhaa wa Hamas
Kwa upande wake jeshi la Israel limesema kwenye taarifa yake leo Jumapili kwamba vikosi vyake vimeyashambulia karibu maeneo 100 kwenye Ukanda wa Gaza na kuwaua wanamgambo wa Hamas.
Limesema pia limeharibu maeneo yanayotumika kufyetua maroketi yaliyovurumishwa siku za hivi karibuni kuelekea Israel.
Wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz alionya juu ya shambulio kali la Israeli iwapo mashambulio ya maroketi kutoka kundi la Hamas yataendelea.
Mashambulizi hayo ya maroketi kutokea Gaza yameripotiwa wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kutafuta makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka na usitishaji mapigano yakiwa yameanza tena nchini Qatar.
Wapatanishi wa Qatar, Misri na Marekani wanashirikiana kwa miezi kadhaa katika juhudi za kufikia makubaliano ya kumaliza vita na kuhakikisha kuachiliwa kwa makumi ya mateka lakini hatua hizo hazijazaa matunda.
Wawakilishi wa israel kwenye mazungumzo hayo walikwenda Doha siku ya Ijumaa kujaribu kufikia makubaliano huku utawala wa Rais Joe Biden, unaojaribu kufanya upatanishi, umelitolea mwito kundi la Hamas kukubali mkataba ulio mezani.
Hamas kwa upande wake imesema iko tayari kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo lakini haijawa wazi iwapo pande hizo mbili zimekaribia kiasi gani kupata mkataba.