Vyombo vya dola Myanmar vyapambana na waandamanaji
26 Septemba 2007Watawa wote hao 17 walijeruhiwa kutokana na mko´ngoto wa polisi wakiwa na virungu,pale walipowakabili waandamanaji karibu na Shwedagon Pagoda kituo muhimu kwa waumini wa dini ya Bhuda nchini humo. Miongoni mwa watawa waliojeruhiwa ni mzee mwenye umri wa miaka 80 aliyesema kwamba alipigwa kirungu kichwani na wanajeshi, wakati wa purukushani hiyo.
Mtawa huyo mwenye umri mkubwa kabisa amekua akishiriki katika maandamano hayo kila siku katika mji mkuu Yangon uliokua ukiitwa zamani Rangoon,tangu yalipoanza siku nane zilizopita, licha ya kwamba hawezi kutembea na imebidi abebwe.
Maafisa wa hospitali wamekataa kutaja idadi ya waliojeruhiwa katika mkon´goto huo ulioendeshwa na vyombo vya dola.Katika mji wa Ahlone kiasi ya watawa 300 waliokua wakiandamana walizuiwa na wanajeshi waliokua na silaha walioanza kupiga risasi za onyo hewani .
Watawa hao wamewataka raia kujitenga na maandamano yao, lakini risasi zilipoanza kusikika, mamia ya watu walilala chini, wakiendelea kuonyesha mshikamano na watawa hao. Katika hatua ya kupambana na maandamano hayo jana watawala nchini Myanamar walitangaza amri ya kutotoka nje kuanzia magharibi hadi alfajiri.
Katika mtaa wa Sule Pagoda, wanajeshi walijaribu kutumia hewa ya kutoa machozi kuutawanya umati wa waandamanaji, lakini maelfu walijiunga na watawa wakirudi tena kukusanyika upya. Baadhi ya waandamanaji walianza kuwarushia mawe wanajseshi waliojibu kwa risasi za onyo. Mtu mmoja alionekana akiondolewa baada ya kujeruhiwa wakati umati wa watu ulipokua ukikimbia pale wanajeshi walipotumia hewa ya kutoa machozi kuwatawanya.
Wito wa baadhi ya viongozi wa kimataifa wa hatua dhidi ya watawala wa Myanmar unazidi. Leo waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown aliwaambia waandishi habari katika mkutano mkuu wa chama chake cha Leba mjini Bournemouth,kwamba anatoa wito wa kikao maalum cha baraza la usalama la umoja wa mataifa kuzungumzia matukio nchini Myanmar, na akawataka watawala wa kijeshi kujizuwia na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji. Alisema anataka kuuona ulimwengu ukiliya shughulikia matukio haya, na kwamba ni muhimu kuweko na shinikizo la kimataifa.
Kwa upande mwengine Wa-Myanmar wanaoishi uhamishoni wameitaka serikali ya Ujerumani kutoa mbinyo wa kisiasa kwa watawala wa kijeshi nchini mwao. Ofisi ya Burma na jumuiya ya dini ya Budha-Sasana Ramsi, zimetoa wito wa vikwazo vya kiuchumi na kuvunjwa kwa uhusiano wa kibalozi, ikiwa wanajeshi watayavunja maandamano ya amani nchini humo.
Katibu mkuu wa ofisi hiyo ya Burma Htoo Min alisema hali huko Myanmar ni mbaya lakini wakati huo huo ni ya kutia moyo. Alisema watawa wanaoandamana kwa siku ya nane dhidi ya utawala wan chi hjiyo, ni watu wenye kuheshimiwa sana na wana utamaduni wa muda mrefu wa kukosoa na kupinga maovu.