Waandamanaji wadai ushindi Uturuki
2 Juni 2013Makundi ya haki za binadamu yameshutumu matumizi ya nguvu yaliyofanywa na polisi, huku shirika la Amnesty International likisema kuwa watu wawili wameuawa, wakati mataifa washirika wa Uturuki ya magharibi Uingereza na Marekani zikitoa wito kwa serikali kuonesha uvumilivu.
Uwanja wa Taksim umekuwa katikati ya wimbi la maandamano ambayo yamesababisha watu kadha kujeruhiwa, kwa mujibu wa Amnesty International mamia wamejeruhiwa, ambapo pia baadhi ya waandamanaji wamebakia kuwa hawaoni kutokana na gesi ya kutoa machozi kutokana na mabomu ya polisi.
Waandamanaji watamba
Jioni ya Jumamosi, hata hivyo, waandamanaji walicheza na kuimba katika uwanja huo baada ya polisi kujiondoa kutoka katika eneo hilo, na wengine kufyatua fataki katika kusherehekea.
"Serikali ijiuzulu!" waandamanaji walipiga kelele wakati polisi wakirejea nyuma. "Tuko hapa tayyip, wewe uko wapi?" Waliimba , wakimbeza waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan.
Kile kilichoanza kama malalamiko dhidi ya mradi wa serikali ya mtaa umeingia katika maandamano makubwa dhidi ya kile wakosoaji wanachosema kuwa ni agenda ya uhafidhina na mkono wa chuma.
Ghasia zasambaa
Tangu mapambano ya mwanzo siku ya Ijumaa, ghasia zimesambaa katika miji mingine nchini humo. Jana Jumamosi(01.06.2013), polisi mjini Ankara walilizuwia kundi la waandamanaji kulifikia jengo la bunge pamoja na ofisi ya waziri mkuu.
Erdogan amekiri katika hotuba kuwa kumekuwa na hatua nyingine za matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa polisi.
Lakini ameongeza: "Nawatolea wito waandamanaji kuacha maandamano mara moja." Wizara ya mambo ya ndani imesema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya maafisa wa polisi ambao wamefanya mambo ambayo ni kinyume na sheria.
Erdogan alikuwa akizungumza wakati machafuko hayo yakiendelea kwa siku ya pili mfululizo katika uwanja wa Taksim, eneo maarufu la kitalii na kwa kawaida hutumika pia kwa mikutano mjini Istanbul.
Hata hivyo waandamanaji wamewasha mioto na kupambana na polisi katika baadhi ya sehemu za mji wa Istanbul na Ankara mapema leo Jumapili, lakini mitaa imekuwa kwa wastani shwari baad ya siku mbili za maandamano makubwa na ghasia nchini Uturuki dhidi ya serikali ya nchi hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri : Bruce Amani.