Waangalizi uchaguzi wajizuia kutoa msimamo wa uchaguzi Kongo
29 Desemba 2023Ripoti ya awali iliyotarajiwa sana ya ujumbe wa uchunguzi wa Kanisa Katoliki na la lile la kiprotestanti nchini Kongo ilitolewa kwenye hafla iliohudhuriwa na mabalozi wa nchi za nje mjini Kinshasa.
Ripoti hiyo ya waangalizi 25,000 wa uchaguzi waliotumwa katika vituo vyote vya kupigia kura katika nchi nzima ,imesema visa takriban elfu tisa vinaonyesha hitilafu za upigaji kura.
Miongoni mwa kasoro zilizotajwa na waangalizi wa kanisa katoliki na lile la kiprotestanti ni pamoja na kucheleweshwa kwa upigaji kura ambao kulisababisha watu wengi kutojitokeza kupiga kura. Ripoti hiyo imesema ni salimia 26 pekee ya vituo vilivyofungua kwa wakati. Ripoti inaelezea poia ubovu wa mashine za kupiga kura ambazo asilimia kubwa haizikuweza kufanya kazi.
Ujumbe huo uligundua visa vingi vya ukiukwaji wa taratibu za upigaji kura ambavyo huenda vikaathiri uadilifu wa matokeo ya kura mbalimbali katika maeneo tofauti.
Uwazi wa tume ya uchaguzi mashakani ?
Askofu Donatien Nshole, msemaji wa Kongamano la maaskofu wa Kongo na kiongozi wa ujumbe huo wa pamoja wa makanisa, amesema kurefusha rasmi uchaguzi huo kwa zaidi ya siku moja ni kinyume cha sheria za uchaguzi.
''Kwa kuzingatia mazingira ambayo upigaji kura ulifanyika, waangalizi wa makanisa katoliki na kiprotenstanti inaiomba tume ya uchaguzi CENI hasa, ili kuzipa imani pande mbalimbali zinazohusika katika mchakato huu, kutaja idadi ya vituo vilivyofunguliwa tarehe 20 Desemba 2023 na vile vilivyofunguliwa baada ya tarehe hiyo.", alisema Nshole.
''Kulikuwa na matatizo''
Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya, amesema matokeo ya uchaguzi wa wiki iliyopita hayatafutwa licha ya miito inayojirudia kutoka kwa wagombea wa upinzani kutaka uchaguzi wote urudiwe.
"Sote tuligundua kuwa kulikuwa na matatizo. Kulikuwa na maeneo ambapo vituovya kupigia kura vilifunguliwa kwa kuchelewa. Kulikuwa na maeneo ambapo mashine hazikufika kwa wakati. Kulikuwa na maeneo mengine ambapo kulikuwa na matatizo ya mashine. Lakini hapa, lazima pia tutambue shauku kubwa wa Wakongo ambao, kwa wengine, walisubiri masaa 10 hadi 12 foleni ili kupiga kura.'', alisema Muyaya.
Bila kutoa maelezo zaidi, makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti yalithibitisha kwamba mgombea mmoja urais alikuwa akiongoza vyema, akishinda zaidi ya nusu ya kura zilizohesabiwa, kulingana na hesabu yao wenyewe. Tume ya uchaguzi imetarajiwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais Jumapili ya Desemba 31, kabla ya Mahakama ya katiba kuidhinisha matokeo hayo Januari 10.