1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLiberia

Waangalizi wa kimataifa waipongeza Liberia kwa uchaguzi wake

Josephat Charo
13 Oktoba 2023

Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya, Andreas Schieder amesema siku ya uchaguzi ilikuwa tulivu na uchaguzi uliandaliwa vyema.

https://p.dw.com/p/4XUce
Liberia Wahl 2023
Picha: John Wessels/AFP

Waangalizi wa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS na Umoja wa Ulaya wameipongeza Liberia kwa kufanya uchaguzi wa amani wa rais na bunge siku mbili zilizopita.

Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya, Andreas Schieder amesema siku ya uchaguzi ilikuwa tulivu na uchaguzi uliandaliwa vyema na tume ya kitaifa ya uchaguzi na maafisa wake kote nchini.

Tume ya Umoja wa Ulaya imesema kampeni zilifanyika kwa amani kwa kiwango kikubwa na vyombo vya habari vilifanikiwa kufanya kazi yao kwa uhuru. Hata hivyo, Schieder amesema utumiaji wa majukwaa ya serikali na raslimali za dola ulimsaidia rais wa sasa George Weah anayetaka kuendelea kuiongoza Liberia.

Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza tangu Umoja wa Mataifa ulipokamilisha tume yake ya amani nchini Liberia mnamo 2018.