Waangalizi wa Umoja wa Mataifa waondoka Syria, mauaji yaendelea
20 Agosti 2012Katika mkutano wake na waandishi wa habari hapo jana, mkuu wa timu ya waangalizi hao, Jenerali Babacar Gaye, alizilaumu pande zote mbili kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano.
“Ndiyo tumefadhaishwa sana, kwa sababu wito wa kumaliza ghasia haukusikiwa na pande zote mbili. Pande zote mbili zina wajibu chini ya sheria za kimataifa kuhakikisha kuwa raia wanalindwa. Wajibu huo haukuheshimiwa.” Alisema Jenerali Gaye.
Mapigano yanaendelea kuripotiwa katika miji kadhaa nchini Syria, ikiwemo Aleppo na Damascus. Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza, limesema miili ya watu 16 katika kijiji cha al-Tall kwenye jimbo Damascus, ikiwemo ya watoto wadogo. Jana peke yake, ambayo ilikuwa ni sikukuu ya Eid el-Fitr, wanajeshi 34, raia 28 na waasi 22 waliuawa nchini kote.
Mjini Aleppo, waasi wanadai kupata ushindi baada ya kuviondosha vikosi vya serikali katika mitaa kadhaa ya mji huo. Taarifa hizo hazijathibitishwa na vyombo huru vya habari.
Brahimi: Kazi si kuepusha vita, ni kuvisimamisha
Rais Assad alijitokeza hadharani hapo jana kwenye sala ya Idd mjini Damascus, huku maandamano yakiendelea kwenye mitaa ya mji huo dhidi ya utawala wake.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa aliyeteuliwa kuchukuwa nafasi ya Kofi Annan, Lakhdar Brahimi amesema kinachotakiwa kufanyika nchini Syria si kuepusha vita visitokee, bali na kuvisimamisha, kwani tayari vimeshaanza na vinaendelea.
Katika hatua nyengine, meli ya kijasusi ya Ujerumani inaripotiwa kuwapo kwenye bahari ya Mediterranean kuungana na vyombo vyengine vya kimataifa vinavyofuatilia taarifa za kijeshi za Syria katika eneo hilo.
Tayari shirika la ujasusi la Uingereza limeweka kituo chake nchini Cyprus ambako linafuatilia kwa karibu mambo yanavyoendelea Syria. Taarifa zinazokusanywa na vyombo hivyo hupelekwa Marekani na Uturuki ambako nako hurudishwa kwa waasi wa Syria.
Kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa
Kuondoka kwa waangalizi hao wa Umoja wa Mataifa kunatajwa kama moja ya matukio mabaya kabisa ya kufeli kwa taasisi hiyo kubwa duniani, kunusuru damu ya maelfu ya wanawake, watoto na watu wasiojiweza kumwagwa.
Umoja wa Mataifa, hata hivyo, umepanga kuendelea kuwa na ofisi yake ya kisiasa mjini Damascus kusaidia juhudi za upatanishi za mrithi wa Annan, mwanadiplomasia wa Algeria, Lakhdar Brahimi.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema ofisi hiyo huenda ikawa na wafanyakazi kati ya 20 na 30 wakiwemo wataalamu wa siasa, misaada ya kibinaadamu na masuala ya kijeshi.
Kile kilichoanza mwezi Machi mwaka jana kama maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Assad, kimegeuka kuwa uasi mkubwa nchini kote baada ya jeshi na vikosi vya usalama kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya raia. Zaidi ya watu 23,000 wameshauawa, kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye m akao yake nchini Uingereza.
Mwandishi: Björn Blaschke/Mohammed Khelef/DW
Mhariri: Josephat Charo