1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi 78 wauawa Syria

26 Oktoba 2020

Mashambulizi ya ndege yaliyofanywa na Urusi ambayo ni mshirika wa serikali ya Syria yamewauwa waasi 78 wanaoungwa mkono na Uturuki kaskazini magharibi mwa Syria.

https://p.dw.com/p/3kSSw
Nahostkonflikt - Tote nach Luftangriff in Syrien
Picha: Moawia Atrash/dpa/picture alliance

Ndege hizo za Urusi zimewauwa waasi 78 na kuwajeruhi watu wengine  90 wakati zilipolenga kambi za mafunzo inayosimamiwa na kundi la Faylaq al-Sham  katika eneo la Jabal Duwayli lililoko jimbo la Idlib, hii ikiwa ni kulingana na shirika la haki za binaadamu linalofuatilia mzozo nchini humo.

Mapema mwezi Machi, makubaliano yaliyofikiwa kati ya Urusi  na Uturuki yalihitimisha mashambulizi mabaya na ya muda mrefu ya kijeshi yanayoungwa mkono na Urusi katika ngome hiyo ya mwisho ya waasi katika jimbo la Idlib.

Mashambulizi hayo ya tangu Disemba yalisababisha watu karibu milioni moja kuyakimbia makazi yao katika mzozo huo ambao ni mmojawapo ya mibaya kabisa ya kibinaadamu uliosababishwa na vita vya miaka tisa vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Rami Abdel Rahman
Rami Abdel Rahman, mkuu wa shirika la haki za binaadamu linaloufuatilia mzozo wa SyriaPicha: Getty Images/AFP/L. Neal

Mkuu wa shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman ameyaelezea mashambulizi hayo kuwa ni mabaya zaidi tangu makubaliano ya kusitishwa mapigano yalipoanza kutekelezwa na kulingana naye yamesababisha vifo vya watu 100. Inatarajiwa idadi ya vifo kuongezeka kwa kuwa wengi wa majeruhi wako katika hali mbaya.

Hayo yanatokea wakati hapo jana, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Geir Pedersen akisema anataraji kwamba makubaliano ya msingi yanaweza kufikiwa na yatakayosaidia kuupeleka mbele mchakato wa kisiasa nchini humo.

Amesema "Watu wa Syria wamekuwa wakiishi katika kipindi kigumu sana. Wamekuwa wakiteseka sana. Kwa kweli kuna njia moja tu ya kutatua hili nalo ni kuanza kutekeleza azimio la Baraza la Usalama na kuanza kuzingatia mchakato wa kisiasa."

UN-Sicherheitsrat verlängert Syrienhilfe eingeschränkt
Wengi wameyakimbia makazi yao, na sasa wanaishi kwenye makambi, ingawa baadhi ya raia wamerudi IdlibPicha: picture-alliance/dpa/A. Alkharboutli

Kundi la wanamgambo la National Liberation Front, NFL linalojumuisha waasi wanaoungwa mkono na Uturuki na waliojikita Idlib ambalo pia linawajumuisha Faylaq al-Sham, linaloyaunganisha makundi 19 ya waasi wa Kiislamu wa madhehebu ya Sunni yanayosaidiwa na Uturuki limeliambia shirika la habari la AFP kwamba shambulizi hilo la Jumatatu lililofanywa na Urusi limepiga moja ya maeneo yake na kusababisha vifo na majeruhi. Hata hivyo halikutoa idadi kamili ya vifo.

Msemaji wa NFL Dayf Raad amelaani mashambulizi hayo ya kijeshi ya Urusi kwa kushirikiana na vikosi vya serikali ya Syria ambayo amesema yameendelea kukiuka makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Uturuki na Urusi kwa kulenga kambi za kijeshi, vijiji na miji.

Kundi hilo la Faylaq al-Sham limekuwa likijiandaa kufanya mahafali katika siku chache zijazo ya wanamgambo wapya takriban 150 waliofunzwa kwenye kambi hiyo. 

Mashambulizi ya ndege ya Urusi mara kwa mara yamelenga kambi za kijeshi, ikiwa ni pamoja na zile za makundi yanayoungwa mkono na Uturuki, amesema Abdel Rahman.

Mashirika: AFPE/DPAE