Waasi Libya waendeleza mapambano
28 Aprili 2011Waasi mjini Misrata wamejigamba wanakaribia kuurejesha uwanja huo wa ndege katika himaya yao. Mkuu wa Kamati ya Mpito ya waasi mjini humo, Khalid Azwawi amewaambia waandishi wa habari kwamba wapiganaji wao wamemudu kupambana na wanajeshi ya Gaddafi na kuwaondoa nje ya mji huo.
Lakini akaongeza kuwa kwa hivi sasa hawako mbali ndio maana wanajaribu kurushia makombora katika eneo la bandari.
Hata hivyo awali habari kutoka Benghazi zilisema waasi 7 wameuwawa na wanajeshi wa Ghaddafi katika mapambano yaliyotokea usiku wa kuamkia leo katika mji huo huo wa Misrata.
Wanajeshi watiifu kwa Ghadafi walikishambulia kituo kimoja cha ukaguzi karibu na eneo la mapambano kwa makombora mazito ya mizinga na roketi.
Wakati huo huo ujumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa unaoongozwa na Abdul Ila al-Khatib, unafanya mazungumzo nchini Uturuki kabla ya kuelekea makao makuu ya waasi mjini Benghazi.
Khatib na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema wanajadili hali ya machafuko maeneo ya Kaskazini mwa Afrika.
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon alisema bado ofisi yake ina matumani ya kusitishwa kwa mapigano nchini Libya.
Akizungumza juu ya mzozo wa Libya, waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de maiziere, amesema. "Tunashiriki katika mchakato huu wa kisiasa kwa sababu sisi tupo katika jopo la mawasiliano, tunaunga mkono vikwazo madhubuti dhidi ya Libya na kama Umoja wa Mataifa utahitaji misaada ya kibinaadamu tutakuwa tayari."
Nayo Urusi imesema haina mpango wa kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili kile ambacho imekiita kuwa ni ukandamizaji wa nchi za magharibi dhidi ya Libya.
Habari hizo zilizotangazwa na Shirika la Habari la nchini humo la TASS limeinukuu taarifa ya wizara ya mambo ya nje.
Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin ameikosoa operesheni ya kuzuia ndege kuruka nchini Libya inayotekelezwa na nchi za magharibi kwa kusema imevuka mipaka ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mapema jana Libya iliomba Urusi kuitisha mkutano wa dharura wa baraza hilo. Lakini kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Gennady Gatilov amekanusha kupanga mkutano huo.
Urusi ina kura ya turufu kama mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakini mwezi uliopita haikupiga kura azimio la baraza hilo la kutumika nguvu kuwalinda raia nchini Libya.
Jitihada za uokoaji zinaendelea ambapo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema Alhamisi iliyopita limefanikiwa kuwaokoa wakimbizi 935 na kuwapeleka Bengazi licha ya kuwepo kwa mashambulizi makali mjini Misrata.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/RTR
Mhariri: Josephat Charo