Waasi wa Kihouthi wafanya mashambulizi zaidi Saudi Arabia
26 Machi 2021Saudi Arabia imesema leo kuwa tanki la mafuta katika kituo kimoja cha mafuta nchini humo liliwaka moto baada ya kulengwa na kombora na kwamba shambulio hilo linakuja wakati wa kumbukumbu ya miaka sita ya taifa hilo kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu vya Yemen.
Shambulio hilo huko Jizan kusini magharibi mwa Saudi Arabia karibu na mpaka na Yemen limefanywa na kile maafisa wa ulinzi nchini humo wameelezea kuwa mkusanyiko wa ndege nane zisizo na rubani zilizokuwa zimebeba mabomu. Katika taarifa iliyopeperushwa kupitia televisheni hii leo, msemaji wa kundi hilo la Kihouthi Yahya Serae amesema kuwa kundi hilo lililenga maeneo ya taasisi kadhaa za shirika la mafuta la Aramco linalomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia katika miji ya Jizan, Ras Tanura, Yanbu na Rabigh kwa kutumiandege 18 zisizo na rubani na makombora manane .
Serae ameongeza kuwa ndege nyingine sita zisizo na rubani zilizinduliwa kama sehemu ya operesheni kubwa dhidi ya ngome za kijeshi katika maeneo ya mipaka ya Saudi Arabia ya Najran na Asir na kwamba operesheni hii imetimiza malengo yake kwa ufanisi na wanathibitisha kuwa wako tayari kufanya mashambulio zaidi mabaya katika siku zijazo bila ya kutoa habari zaidi. Serae amesema kuwa mashambulio hayo yameadhimisha mwanzo wa mwaka wa saba wa muungano wa kijeshi unaaongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen.
Taifa hilo la kifalme limekabiliwa na idadi inayoongezeka ya mashambulio kama hayo na kasi yake haijapungua tangu ilipopendekeza mkataba wa kusitisha mapigano kwa kundi hilo la Kihouthi siku ya Jumatatu. Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliingia nchini Yemen Mnamo Machi 25 mwaka 2015 wakati kundi la Kihouthi lilipotishia kuuteka mji wa bandari wa Yemen, Aden, na kuipindua serikali inayotambulika kimataifa.
Saudi Arabia iliahidi kuwa mashambulio hayo ambayo yalikuwa wazo la mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman yangemalizika katika muda mfupi. Miaka sita baadaye, mapigano bado yanaendelea . Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia matukio katika maeneo ya mizozo, mapigano hayo hayo yamesababisha vifo vya watu elfi 130 wanaowajumuisha zaidi ya raia elfu 13 waliouawa katika mashambulio ya kulengwa. Maelfu ya watoto pia wamekufa kutokana na ukosefu wa chakula na magonjwa.