Waasi wa Kijerumani wauawa Pakistan.
5 Oktoba 2010Waapiganaji hao wenye itikadi kali walikufa baada ya makombora wawili kutoka kutoka katika ndege zinazoshukiwa kuwa za Marekani zinazojiendesha zenyewe bila ya rubani za shirika la Kijasusi la CIA, kushambulia msikiti katika mji wa Mir Ali kaskazini mwa Waziristan.
Maafisa usalama wa Pakistan wamesema wapiganaji hao ni wanachama kutoka katika kundi linalojulikana kama Jihad Islami na kwamba ni Wajerumani wenye asili ya Uturuki.
Lakini bila ya kuitaja idadi kamili, afisa mwingine wa usalama nchini humo amesema baadhi ya wapiganaji raia wa bara la Ulaya wakiwemo Wajerumani, waliuawa katika shambulio hilo.
Eneo la kaskazini mwa Waziristan ni maarufu kwa kuwa kificho cha wapiganaji wa Taliban na al Qaeda.
Wapiganaji wengine watatu waliuawa pia katika shambulio hilo.
Hata hivyo hivyo mkazi wa eneo la Mirali, lilipotokea shambulio Mohammad Alam ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba shambulio hilo lilitokea wakati watu wakiwa wamekusanyika msikitini kwa ajili ya ibada.
Amesema eneo hilo lilizingirwa na wapiganaji, baada ya shambulio hilo, na kwamba walikuwa hawaruhusu mtu yoyote.
Shambulio hilo limekuja siku moja baada ya Marekani na Uingereza kuonya juu ya kuongezeka kwa hatari ya mashambulio ya kigaidi barani Ulaya.
Wizara ya Mambo ya Nchi za nje ya Marekani iliwaonya raia wa nchi hiyo kuchukua tahadhari iwapo watatembelea bara la Ulaya. huku Uingereza nayo ikiwa pia imeongeza kiwango cha tahadhari kwa safari za Ufaransa na Ujerumani.
Maafisa wa usalama wa nchi za magharibi walisema wiki iliyopita kwamba wanaamini kundi la wapiganaji lililoko kaskazini mwa Pakistan linapanga kupanga mashambulizi.
Kituo cha televisheni cha Marekani cha Fox News, kimemnukuu afisa mmoja wa upelelezi ambaye hajatajwa jina lake, akisema kuwa wapiganaji wameorodhesha maeneo yanayolengwa nchini Ufaransa na Ujerumani, ikiwemo mnara maarufu wa Eiffel, wakati katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, lango la Brandenburg ndio linalolengwa pamoja na kituo kikuu cha treni.
Marekani imeongeza kufanya mashambulio ya anga katika maeneo ya wapiganaji, kaskazini magharibi mwa Pakistan, wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda, ambapo katika kipindi cha mwezi uliopita wa Septemba pekee walifanya mashambulio 21, idadi ambayo ni kubwa katika kipindi cha mwezi mmoja.
Hata hivyo bado haijafahamika wazi jinsi mashambulio hayo yanavyoingilia na ripoti za kupanga mashambulio ya kigaidi barani Ulaya.
Katika hatua nyingine Pakistan imeonya kwamba mashambulio hayo yanayofanywa nchini humo, yanaweza kuhujumu juhudi za kufikia makubaliano na wapiganaji , kutokana na madhara wanayoyapata raia, kuusababisha hasira ya umma na hatimaye kuwaunga mkono wapiganaji.
Halima Nyanza(AFP,Reuters)
Mpitiaji:Mtullya abdu.