Waasi wa Libya waahidiwa mabilioni ya dola
10 Juni 2011Katika mkutano uliofanyika Abu Dhabi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amesema kuwa Marekani inashirikiana na nchi nyingine kimataifa, kupitia Umoja wa Mataifa, kupanga kuhusu Libya baada ya kuondolewa Gaddafi.
Clinton aliongeza kuwa shinikizo la jeshi la kimataifa, la kiuchumi na kisiasa, linazidi kwa kiongozi wa Libya ajiuzulu madarakani.
Katika kuunga mkono upinzani, Marekani iliungana na Australia na Uhispania katika kulitambua baraza la kimataifa la waasi nchini Libya kama mwakilishi halali wa wananchi wa Libya.Hillary Clinton alisema kuwa siku za Gaddafi ni za kuhesabika.
Clinton alikutana na wanachama wenzake wa shirika la kujihami la NATO na nchi nyingine zinazoshiriki katika mashabulio dhidi ya vikosi vya Gaddafi , katika mazungumnzo ya awamu ya tatu kuhusu Libya.
Hatahivyo, Clinton hakutoa msaada wa moja kwa moja wa kifedha kwa waasi wa Libya, badala yake aliahidi dola milioni 26.5, kwa wahanga wa mzozo nchini humo, wakiwemo wakimbizi wa Libya.Huenda fedha hizo zikagawanywa kupitia mashirika ya kutoa misaada.
Lakini waziri wa mambo ya nje wa Italia, Franco Frattini, amesema kuwa nchi yake itawapa waasi hao mikopo na bidhaa za viwanda vya mafuta zenye thamani ya kati ya Euro milioni 300 na 400.Waziri mwenzake wa Ufaransa, Alain Juppe, amesema Paris itatoa Euro milioni 290 ya fedha zilizozuiliwa za Libya, kwa baraza hilo.
Mwanachama mmoja wa baraza hilo la kitaifa nchini Libya amesema kuwa kando kando mwa mkutano huo wa Abu Dhabi, tangu hapo jana, pameanzishwa hazina ya kimataifa ya kuwasaidia waasi hao.
Afisa mmoja kutoka wizara ya mambo ya nje ya Marekani baadaye pia aliwaambia waandishi habari kuwa pamekuwepo ahadi za kiasi ya dola milioni 300 katika mkutano huo, zikiwemo dola milioni 180 kutoka Kuwait, na dola milioni 100 kutoka Qatar.
Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Libya, Abdulrahman Shalgam, amesema baraza la kitaifa la waasi linahitaji kiasi ya dola bilioni 3 katika miezi minne ijayo ili liweze kulipia gharama zake wakati linapigana kumuondoa Muammer Gaddafi.
Mjumbe maalum Mikhail Margelov wa rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, hii leo amesema anajitayarisha kuizuru Tripoli ili kutafuta suluhu kwa mzozo wa Libya baada ya kukutana na upinzani katika mji unaoudhibiti Benghazi.
Katika ishara ya kuzidi shinikizo kwa utawala wa Gaddafi, NATO ilifanya mashambulio mapya hii leo katika mji mkuu wa Tripoli nchini humo, huku miripuko mitatu mikubwa ikitokea mjini Tripoli hapo jana usiku, na kufuatiwa na mengine katika maeneo mengine ya mbali.
Katika siku mbili zilizopita, mashambulio ya NATO nchini Libya yameongezeka tangu kuanza kwa kampeni ya jeshi la kimataifa nchini humo, mnamo Machi 19.
Mwandishi Maryam Dodo Abdalla/Afpe/Ap
Mhariri: Miraji Othman