1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Libya wachukua mji wa Wazin, waandishi wauawa

21 Aprili 2011

Waasi nchini Libya wameuteka mji wa mpakani wa Wazin baada ya kuwashinda wanajeshi wa Muammar Gaddafi, lakini idadi ya raia wanaouawa kutokana na makabiliano ya waasi, wanajeshi na pia maroketi ya NATO inaongezeka.

https://p.dw.com/p/111kI
Tim Hetherington wakati wa uhai wake
Tim Hetherington wakati wa uhai wakePicha: dapd

Mashahidi wanasema kwamba baada ya mapigano yaliyochukuwa muda mfupi asubuhi ya Alhamis, waasi wamefanikiwa kuuchukua mji huo, ambao unapakana na mji wa Dehiba ulioko Tunisia, ukitenganishwa na eneo la mpaka wa kimataifa. Bendera ya ufalme wa Libya, ambayo ilitumika kabla ya Gaddafi kuingia madarakani, sasa ndiyo inayopepea kwenye mji huo.

Lakini wakati waasi wakisherehekea ushindi huo, kituo cha televisheni cha Libya kimeripoti kuwa watu 7 wameuawa na wengine 18 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya NATO ya asubuhi ya leo kwenye eneo la Khallat al-Farjan mjini Tripoli.

Kituo cha al-Jamaahiriyyah kimeripoti kwamba makombora ya NATO yaliharibu majengo kadhaa katika eneo hilo na pia kwenye mji wa Gharyan, ulio kusini mwa Tripoli, ambako nako watu kadhaa wameuawa.

Hakuna chanzo huru kinachoweza kuthibitisha taarifa hii, lakini NATO yenyewe imewataka raia wa Libya kukaa mbali na vikosi vya Gaddafi.

NATO yataka raia wajitenge na vikosi vya Gaddafi

Chris Hondros wakati wa uhai wake
Chris Hondros wakati wa uhai wakePicha: dapd

Taarifa ya NATO iliyotolewa na jenerali mwenye dhamana ya operesheni ya Libya, Charles Bouchard, imesema kwamba wakati hatua za kuwalinda raia zinachukuliwa, maafa pia huwa hayaepukiki.

"Marubani na wanamikakati wetu wanachukua kila jitihada kuhakikisha kuwa tunapunguza kiwango cha maafa kwa raia tunapomshambulia adui, lakini maafa hayawezi kukosekana moja kwa moja. Raia wanaweza kuisaidia NATO kwa kujitenga mbali na vikosi vya Gaddafi na vifaa vyake kila inapowezekana." Amesema Luteni Jenerali Bouchard.

Huko mjini Misrata, ripoti zinasema kwamba hali imezidi kuwa mbaya kutokana na mashambulizi ya vikosi vya Gaddafi. Katika makabiliano kati ya vikosi hivyo na waasi, waandishi wawili wa habari, Tim Hetherington na Chris Hondros waliuawa.

Tim alikuwa mpiga picha wa Uingereza aliyejizolea sifa kutokana na kupiga picha za kwenye maeneo hatari ya vita na alikuwa ameteuliwa kuwania tunzo ya Oscar.

Mwaka 2007 alishinda tunzo ya Picha Bora ya Dunia kwa picha zake za wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan. Mwezake, Chris, alifariki dunia akiwa hospitali. Wapiga picha wengine wawili Guy Martin na Michael Brown, ambao pia walijeruhiwa, bado wanaendelea na matibabu.

Katika hospitali ya mjini Misrata, madaktari wanasema kwamba idadi ya majeruhi wanaoletwa hapo na wanaopoteza maisha wakiwa mikononi mwao inaongezeka. Dk. Mohammed al-Fagieh, wa hospitali ya Shefarzt Hilal, anasema kwamba uwezo wao unazidiwa nguvu.

"Baadhi ya wakati baadhi ya wakati majeruhi wanafikia 50 mpaka 60 kwa siku. Nazungumzia wale wanaoletwa hapa hospitali tu, sio kwa Misrata nzima. Idadi hii huweza kuongezeka mara mbili hadi tatu siku nyengine." Amesema Dk. Al-Fagieh.

Waasi wataka mashambulizi ya NATO yaongezeke

Libyen Misrata Brand Fabrik Aufstand
James Keogh/Wostok Press/MAXPPP Libye, Misrata 15/04/2011 - A company of ceramic Misurata was destroyed as a result of fighting between the insurgents and the troops of Colonel GaddafiPicha: picture alliance / dpa

Wakati huo huo, kiongozi wa waasi, Mustafa Abdel Jalil, amesema kwamba wanategemea mashambulizi zaidi kutoka vikosi vya NATO kuweza kumshinda Gaddafi. Akiwa mjini Paris, alikokutana na Rais Nikolas Sarkuzy hapo jana, Jalil amekiambia kituo cha televisheni cha France 24, kwamba kadiri Gaddafi anavyoendelea kubakia madarakani, ndivyo damu zaidi inapomwagwa.

Waasi wanataka msaada zaidi wa kijeshi ili kusaidia kunusuru maisha ya raia, ambapo madaktari wanasema, zaidi ya watu 1,000 wameshauawa tangu mji huo uzingirwe na vikosi vya Gaddafi.

Msimamo wa jumuiya ya kimataifa kutokupeleka jeshi la miguu nchini Libya, unaonekana kuanza kulegea, ambapo tayari Uingereza, Ufaransa na Italia zimeshasema kuwa, zitapeleka maafisa wa kijeshi katika eneo la Mashariki linaloshikiliwa na waasi, kwa ajili ya kutoa msaada wa ushauri.

Hata hivyo, Marekani imesema kwamba haitoshiriki kwenye mpango huo wa kupeleka washauri wa mambo ya kijeshi nchini Libya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters
Mhariri: Josephat Charo