Waasi wa Libya waendelea kupambana dhidi ya vikosi vya Gaddafi
28 Aprili 2011Moreno Ocampo anaendelea na uchunguzi wake juu ya uhalifu wa ubinadamu unaodaiwa kuendelea nchini Libya kufuatia mapambano yanayoshuhudiwa kati ya vikosi vya Kanali Muammar Gaddafi na waasi wanaosaidiwa na vikosi vya jumuiya ya kujihami ya NATO.Uchunguzi huo wa Ocampo mbali na Kanali Gaddafi na wanawe watatu unawalenga pia maafisa wanne wa Libya akiwemo mwanadiplomasia wa ngazi ya ju Mussa Kussa na aliyekuwa waziri mkuu Abu Zayd Omar Dorda,mkurugenzi mkuu wa shirika la usalama wa ndani nchini Libya.Kwa hivi sasa ndani ya Libya kwenyewe waasi wanaendelea kupambana kuukomboa uwanja wa ndege wa Misrata baada ya kuwasogeza nyuma wanajeshi wa Kanali Gaddafi kutoka kwenye bandari ya mji huo huku viongozi wa kikabila nchini humo wakimtaka Gaddafi aondoke madarakani.Kumesikika mripuko mkubwa mjini Tripoli mara tu baada ya ndege za NATO kuruka kwenye anga ya mji huo mkuu wakati waasi nao wakiomba msaada zaidi wa silaha nzito nzito kutoka nchi za Magharibi wamesema ''Nato imefanya vizuri lakini tunahitaji msaada zaidi kuwamaliza wanajeshi wa Kanali Gaddafi''
Waasi katika eneo hilo la Misrata wamesema wanaimani kwamba wanakaribia kuupata ushindi katika mji huo wa Misrata.Wakati hayo yakiendelea maelfu ya wakimbizi wanaendelea kuyakimbia maeeneo hatari huko Magharibi ya Libya huku wakitoa mwito wa vita kumalizwa haraka kutokana na madhila wanayoyapata zaidi kina mama na watoto katika eneo hilo.
Ama upande mwingine mjini Brussels kumefunguliwa taasisi inayowaunga mkono waasi ikiwa na lengo la kufanikisha mawasiliano kati ya Umoja wa Ulaya na jumuiya ya Nato na waasi wa Libya katika harakati za kuelekea kuikomboa Libya na kuleta demokrasia.
Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE
Mhariri Josephat Charo.