Waasi wa M23 wajitenga na mapatano ya kusitisha mapigano
25 Novemba 2022Msemaji wa kisiasa wa kundi hilo Lawrence Kanyuka ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kuwa M23 ilionya waraka wa mapatano hayo kupitia mitandao ya kijamii, na kwamba hakukuwa na mwakilishi wao kwenye mkutano mdogo wa kilele uliofikia maamuzi hayo, hivyo tangazi hilo haliwahusu.
Aliongeza kuwa kawaida panapokuwa na usitishaji mapigano, makubaliano yake huwa kati ya pande mbili zinazopambana.
Wataalamu waionya Congo kuwajumuisha waasi jeshini
Rais wa DRC Felix Tshisekedi na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta, walihudhuria mkutano huo uliofanyika katika mji mkuu wa Angola, Luanda siku ya Jumatano.
Kwenye mkutano wa waandishi habari mjini Kinshasa siku ya Alhamisi, waziri wa mambo ya nje wa Congo, Christophe Lutundula, alisema leo saa 12 kamili jioni M23 wanapaswa kusitisha mashambulizi yao yote.Kanyuka alisema waasi walitangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja mnamo mwezi Aprili, na anaamini mpango huo ulikuwa unaendelea bado, akisisitiza kuwa endapo serikali haitawashambulia Ijumaa saa 12 jioni au asubuhi, wataendelea kuwepo pale, vinginevyo wanajitetea tu.DRC na Rwanda zapata mwafaka kuhusu vita mashariki mwa DRC
Msemaji huyo wa M23 alisema wao wako tayari wakati kufanya majadiliano ya moja kwa moja na serikali ili kutatua mzizi wa mizozo.
Serikali mjini Kinshasa hata hivyo imekataa kushirika mazungumzo na kundi la M23, ambalo inaliita vuguvugu la kigaidi, maadamu linaendelea kukalia maeneo nchini DRC.
Kundi la M23 limekuwa bwete kwa miaka kadhaa, lakini lilichukuwa tena silaha mwaka jana na limetazamwa tangia mwanzo na serikali ya Congo kama linaloungwa mkono na Rwanda, ambayo hata hivyo inakanusha madai hayo.
Waasi hao hivi karibuni waliteka maeneo makubwa ya kaskazini mwa mji wa Goma, ambao ndiyo mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.
Kenyatta azuru mji wa Goma katikati mwa mzozo wa waasi
Mkutano wa kilele wa Luanda ulihitimishwa kwa makubaliano ya kusitisha uhasama mashariki mwa Congo kuanzia Ijumaa jioni, ukifuatia na kuondoka kwa M23 kutoka maeneo inayoyakalia na kurejea kwenye maeneo yao ya awali.
Endapo waasi hao watakaidi agizo hilo, kikosi cha kikanda cha Afrika Mashariki kinachopelekwa mjini Goma kitawafurusha nje, yalisema makubaliano hayo.