Waasi wa Mali wasitisha madai ya kuwa na taifa lao
5 Desemba 2012Kwa mara ya kwanza utawala wa Mali umekutana na kundi la waasi wa kabila la Tuareg, wanamgambo wa kundi la Ansar Din pamoja na makundi mengine ya wapiganaji wa Kiislamu wenye siasa kali na kukubaliana kuwa kuna haja ya kuwepo mjadala mkubwa wa kitaifa juu ya mzozo unaoendelea nchini humo
Mkutano huo umefanyika katikamji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou chini ya usimamizi wa nchi hiyo na kukubaliana kwamba mazungumzo hayo yatahusisha makundi ya jamii mbalimbali zinazoishi kaskazini mwa Mali. Tamko lililotolewa na Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Burkina Faso Djibril Bassole baada ya mkutano huo linasema kuwa makundi hayo yamekubaliana pia kuachana na uhasama uliopo sasa.
Wameahidi pia kuwa watajizatiti kuhakikisha umoja wa kitaifa unapatikana, uhuru wa mipaka pamoja na serikali ambayo haifuati dini kwa wakati huu ambapo wanajiandaa na mazungumzo hayo.
Mazungumzo hayo ni hatua ya kuzuia uingiliaji wa kijeshi wa wa vikosi vya Umoja wa Afrika ambao unasaidiwa na mataifa ya magharibi. Kundi la wanamgambo wa Ansar-Dine lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida limekubali kulegeza msimamo wake mkali na kuachana na vitendo vya ugaidi.
Ouattara asema hatua za kijeshi ndio muafaka
Wakati makubaliano hayo yakifikiwa mjini Ouagadougou, jana hiyo hiyo huko Paris, Ufaransa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi kwa Nchi za Afrika Mgharibi (ECOWAS), Rais Alassane Qouattara wa Cote d´voire amesema kuwa suala la kuingilia kati kijeshi mzozo unaendelea nchini Mali haliepukiki. Ametoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wake na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Qouattara amesema anafahamu kuwa majadiliano ndio njia bora katika kutatua mizozo lakini kwa sasa anaona uingiliaji wa kijeshi ni hatua inayohitajika kuiokoa Mali kutoka mikononi mwa waasi na makundi ya siasa kali za kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo.
Ameliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha matumizi ya nguvu za kijeshi nchini Mali na kuongeza kuwa vikosi vya Umoja wa Afrika viko tayari kwa kazi hiyo. Msemaji wa Rais Hollande amesema kuwa kiongozi huyo ana mawazo kama hayo ya Quattara kuhusu Mali.
Kupitia msaada wa Umoja wa Ulaya, ECOWAS ina mpango wa kuingilia kijeshi kaskazini mwa Mali kuwaondoa waasi wa Tuareg na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu waliochukua eneo hilo mapema mwaka huu. Kikwazo pekee kilichopo katika utekelezaji wa mpango huo ni ruhusa ya Umoja wa Mataifa ambayo hadi sasa haijatolewa.
Mataifa ya Ulaya yanataka kupeleka watalaamu wa kijeshi kulisaidia kiushauri na utaalamu jeshi la Mali, lakini hawatashiriki moja kwa moja kwenye operesheni za mapambano.
Mwandishi: Stumai George/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Oummilkheir Hamidou