Waasi wa TPLF wadaiwa kupora maghala ya misaada Tigray
1 Septemba 2021Sean Jones, Mkuu wa ujumbe wa shirika la misaada la Marekani USAID ameiambia televisheni ya taifa nchini Ethiopia EBC, kwamba kundi la TPLF limekuwa likIfuata maslahi sana na labda wanaiba kutoka kwa raia, lakini Jones amesema hawana uhakika kuhusu hilo.
Sean Jones amesema walichothibitisha ni kwamba maghala kadhaa ya shirika la USAID yaliporwa na kumwagwa kabisa katika maeneo hayo, haswa Amhara, ambako wapiganaji wa TPLF wamethibiti.
Shirika la habari la Ufaranra AFP limesema msemaji wa wapiganaji wa TPLF hakuweza kupatikana kwa kutoa maoni yake kufuatia tuhuma hizo.
Juhudi za kidiplomasia
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed alitupilia mbali miIto ya mapema ya Umoja wa Afrika ya kuweko na mazungumzo baina ya serikali na wapiganaji wa TPLF. Abiy alishikilia msimamo wake kwamba mzozo huo ulikuwa hatua ya kurejesha sheria na utulivu.
Alhamisi Umoja wa Afrika ulitangaza uteuzi wa rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo kuwa mjumbe maalumu wa umoja huo kwa ajili ya Pembe ya Afrika. Ukisema ni sehemu ya mkakati wa kukuza amani, usalama, ustawi na kuwezesha mazungumzo ya kisiasa. Lakini Jumapili, msemaji wa TPLF, Getachew Reda alitupilia mbali uteuzi huo akiutuhumu Umoja wa Afrika kuupendelea upande wa serikali ya Ethiopia na kusema kwamba itakuwa vigumu kutarajia ujumbe huo mpya kuleta mafanikio.
Taharuki za mashirika ya misaada
Tangu mzozo ulipozuka, serikali ya Abiy na waasi wa Tigray wamekuwa wakitupiana lawama juu ya machafuko hayo, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwa kuzuia misafara ya misaada na kusababisha raia kukabiliwa na tatizo la njaa.
Umoja wa Mataifa umekadiria watu laki nne kukumbwa na njaa kwenye jimbo la Tigray. Alhamisi iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA lilisema kuwa usafirishaji wa misaada kwa Tigray ulisitishwa tangu Agosti 20, bila uwezekano wa malori kuingia katika eneo hilo.
Sean Jones amesema shirika lake la USAID limekuwa likitoa msaada wa chakula kwa watu milioni tano kaskazini mwa Ethiopia katika jimbo la Tigray lakini pia sasa katika majimbo ya Amhara na Afar.
Eneo la kaskazini mwa Ethiopia limekumbwa na ghasia tangu Novemba, wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipotuma wanajeshi wake Tigray kupambana na TPLF, chama kinachodhibiti eneo hilo, akidai amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kambi za kijeshi kushambuliwa na waasi hao.