Waasi wanaotaka kujitenga wauwa wanajeshi 14 Pakistan
9 Novemba 2024Bomu hilo liliripuka leo Jumamosi kwenye eneo la abiria katika kituo kikuu cha treni kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Quetta. Msemaji wa Hospitali ya Sandeman mjini Quetta, Wasim Baig, amesema wanajeshi 14 na raia 12 wameuawa.
Mwandishi wa habari wa AFP aliripoti kuona vidimbwi vya damu na mabegi yaliyochanika kwenye eneo hilo, huku paa la jengo la abiria likiporomoshwa chini.
Licha ya mashambulizi ya mara kwa mara kwenye jimbo la Baluchistan, idadi ya waliouawa siku ya Jumamosi ilikuwa kubwa zaidi katika jimbo hilo linalopakana na Afghanistan na Iran na ambalo limekuwa likiwania kujitenga na Pakistan kwa miongo kadhaa.
Soma zaidi: Waasi wauwa 26 Baluchistan
Kundi la wanamgambo wa Baloch Liberation Army (BLA), lilidai kuhusika na mripuko huo, likisema mashambulizi hayo yalielekezwa kwa kikosi cha "jeshi la Pakistan katika kituo cha treni cha Quetta... baada ya wanajeshi hao kumaliza kozi kwenye Chuo cha Kijeshi."
Waziri Mkuu Shehbaz Sharif aliapa kwamba washambuliaji "watakumbana na hatua kali", kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake.