1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yaripotiwa Mashariki mwa Ukraine

Mjahida 10 Machi 2015

Ukraine imewashutumu waasi wanaoiunga mkono Urusi kutumia mabomu na maroketi kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na serikali karibu na mji wa bandari wa Mariupol,ulio katika eneo la Mashariki.

https://p.dw.com/p/1Eo3q
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: AFP/Getty Images/K. Kudryavtsev

Maafisa wa makao makuu ya operesheni za kijeshi nchini Ukraine wamesema wanamgambo wameshambulia maeneo yalioshikiliwa na jeshi la nchi hiyo huku wakijaribu kulisukuma jeshi hilo nje ya eneo la Shyrokyne, kijiji kilichoko kilomita kumi kutoka mji wa Mariupol.

Hata hivyo madai haya hayakuweza kuthibitishwa kwa haraka lakini inaashiria ukiukwaji mkubwa wa makubaliano ya amani yaliotiwa saini tarehe 12 mwezi ulipoita katika mji mkuu wa Belarus Minsk. Mji wa Mariupol ni mji mkubwa eneo la Mashariki mwa Ukraine ulio na idadi ya watu, 500,000 ambao bado uko chini ya udhibiti wa serikali.

Kwa upande mwengine rais wa Ukraine Petro Porohsenko ametangaza kupitia televisheni ya kitaifa kwamba wanajeshi 64 wameuwawa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipoanza kutekelezwa.

Ameongeza kwamba idadi jumla ya wanajeshi 1,549 wameuwawa tangu kuanza kwa mgogoro wa Ukraine miezi 11 iliopita, ambapo Umoja wa Mataifa unakadiria zaidi ya watu 6000 wameuwawa katika mgogoro huo.

Gari la kivita kutoka jeshi la Ukraine
Gari la kivita kutoka jeshi la UkrainePicha: Reuters/G. Garanich

Wakati huo huo Jumuiya ya kujihami NATO imetayarisha operesheni kubwa ya kijeshi Baltic mahali ambapo Urusi inasemekana kujihusisha kwa undani zaidi na vita vya Ukraine.

Aidha maafisa wa jeshi kutoka Marekani wamesema wanajeshi 3000 wameanza kupelekwa katika eneo hilo ambapo shughuli za operesheni za kijeshi zitadumu kwa miezi mitatu. Operesheni hii itaifanya Jumuiya ya NATO kufanya kazi pamoja na washirika wake wa Estonia, Latvia na Lithuania nchi zilizowahi kuwemo katika Umoja wa kisovieti.

Kulingana na Nato Urusi imetumia mwanya uliopo wa kulitwaaeneo la Crimea na kuongeza maradufu uwepo wa jeshi lake katika eneo hilo.

Rais Obama asema juhudi zaidi zinahitajika kuutatua mgogoro wa Ukraine

Kwa upande mwengine rais wa Marekani Barrack Obama na rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk kwa pamoja wametoa wito wa umoja nchini Ukraine pamoja na kuzungumza juu ya changamoto za usalama zinazoikumba bara la ulaya ikiwemo ugaidi.

"Bila ya kuwa na usimamizi na utekelezaji thabiti makubaliano haya hayatakuwa na maana kwahivyo sehemu ya yale tutakayoyajadili itakluwa ni juu ya vipi tutaweza kusimamia utekelzaji kwa ufanisi wa kile kinachoendelea kwenyewe uwanja wa mapambano nchini Ukraine na vipi tutaweza kuendelea kuishinikiza Urusi na waasi ili wayatekeleze makubaliano haya," alisema rais Obama.

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Reuters/K. Lamarque

Umoja wa Ulaya na Marekani wamekuwa wakichukua hatua za pamoja za kuiwekea vikwazo zaidi Urusi kwa kuingilia mgogoro wa Ukraine lakini Rais wa baraza la Ulaya , ambye pia ni waziri mkuu wa zamani wa Poland, Tusk awali alisema kwamba Umoja huo kwa sasa haupo tayari kuweka vikwazo vyengine dhidi ya Urusi huku akisisitiza kuwa kitu muhimu kinachohitajika katika kuutatua mgogoro wa Uklraine ni kuwa na Umoja.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman