1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Wasonga mbele Jamhuri ya Afrika kati

24 Desemba 2012

Waasi katika Jamhuri ya Afrika kati, wameuteka mji wa Bambari, licha ya mwito wa mazungumzo uliotolewa na viongozi wa mataifa ya Afrika ya kati wanaowataka waasi wayahame maeneo wanayoyadhibiti.

https://p.dw.com/p/178Qn
Eneo la kati la mji mkuu wa jamhuri ya Afrika Kati-BanguiPicha: DW/Leclerc

"Baada ya mapambano yaliyodumu saa moja, mji wa Bambari umeangukia mikononi mwa waasi," amesema shahidi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe. Kwa mujibu wa shahidi huyo, vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Afrika kati - FACA, vilikuwa vinasonga mbele kuelekea Bria, mji ulioangukia mikononi mwa waasi wa Seleka tangu Jumanne iliyopita, lakini kilomita tano tu kaskazini ya Bambari, waasi walianza kushambulia na mapigano kuenea hadi katikati ya mji huo.

"Vikosi vya serikali vimerejea nyuma kuelekea Grimari, kilomita 40 toka Bambari," amesema kwa upande wake askofu Edouard Mathos wakati wa mahojiano ya simu pamoja na shirika la habari la Ufaransa, AFP.

Bambari, mojawapo ya miji muhimu ya Jamahuri ya Afrika kati na mji mkuu wa jimbo la Ouaka, ni mojawapo ya ngome za vikosi vya serikali, FACA.

Waasi Wadai makubaliano ya Awali yaheshimiwe

Kamerun Zentralafrikanische Republik Flüchtlinge in Kousseri
Wakimbizi katika kambi ya KousseriPicha: AP

Seleka, muungano wa makundi tofauti ya waasi, unadai miongoni mwa mengineyo, yaheshimiwe makubaliano tofauti ya amani yaliyotiwa saini kati ya mwaka 2007 na 2011, yanayozungumzia utaratibu wa kuwapokonya silaha waasi na kuwajumuisha jeshini.

Viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuia ya uchumi ya Afrika Kati waliokutana N'Djamena nchini Chad ijumaa iliyopita, waliridhia mwito wa waasi wa kujadiliwa upya makubaliano tofauti ya amani yaliyofikiwa. Hata hivyo wamewataka kwanza waasi warejee katika vituo vyao vya awali mnamo muda usiopindukia wiki moja.

Seleka wanaipinga fikra hiyo wanasema hawawezi kurejea nyuma kabla ya kufikiwa makubaliano ya kuweka chini silaha.

Msemaji wa waasi, Eric Massi, amesema kutekwa miji ya Ndassima na Ippy ni jibu kwa uchokozi wa vikosi vya serikali, FACA.

"Rais Francois Bozizé hana dhamira ya kuheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha na ikiwa vikosi vyake vitaingia huku, hatutakuwa na njia nyengine isipokuwa kujibu uchokozi wao," amesema msemaji huyo aliyemtuhumu kiongozi wa vikosi vya jeshi la serikali kuwaamuru wanajeshi wake waujongelee mji wa Bria waliouteka tangu Jumanne iliyopita.

Tchad yajitolea kupatanisha

François-Bozizé Präsident der Zentralafrikanischen Republik
Rais François-Bozizé wa Jamhuri ya Afrika katiPicha: AP

Nchi jirani ya Chad imejitolea kupatanisha. Wiki iliyopita ilituma wanajeshi ili kuzuwia mapigano kati ya pande mbili zinazohasimiana na sio kupigana. Serikali ya Chad sawa na serikali ya Jamhuri ya Afrika kati hazijasema chochote hadi wakati huu, kwa hivyo ni shida kuashiria wanajeshi wake wanapanga kufanya nini katika wakati ambapo vikosi vya FACA, ambavyo havina vifaa wala motisha, havionyeshi kuwa na nguvu za kutosha kupambana na waasi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo