Waasi watimuliwa Khan Shaikhoun nchini Syria
20 Agosti 2019Kukombolewa maeneo hayo ni ushindi mkubwa kwa rais Bashar al Assad katika eneo la kaskazini magharibi ambayo ndio ngome ya mwisho kubwa ya waasi wa Syria.
Shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam lenye makao yake nchini Uingereza na wanaharakati katika maeneo hayo wamesema waasi wameuhama mji huo, Khan Sheikhoun ,baada ya hujuma kali za mabomu.
Vikisaidiwa na ndege za kivita za Urusi, vikosi vya serikali ya rais Bashar al Assad vimefanikiwa kuingia katika mji huo mnamo saa za usiku jana. Kwa mujibu wa wanaharakati, wanajeshi hao wa serikali wanapiga doria kuwasaka waasi na miripuko iliyofichwa chini ya ardhi.
Waasi wanadai mapigano yanaendelea
Kundi la waasi wenye nguvu zaidi katika eneo hilo, Hayat Tahrir al-Sham linasema hata hivyo waasi wanaendelea kudhibiti sehemu ya mji wa Khan Shaikhoun na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Hama baada ya hujuma za mabomu kusita.
Hakuna bado ripoti zozote zilizotolewa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya Syria.
Vikosi vya serikali ya Syria vimeanzisha hujuma za kijeshi dhidi ya waasi katika eneo la kaskazini magharibi tangu mwezi April uliopita, opereshini zilizoangamiza maisha ya mamia ya watu na kuwalazimisha malaki kukimbilia katika eneo linalopakana na Uturuki.
Mji wa Khan Shaikhoun umekuwa ukidhibitiwa na waasi tangu mwaka 2014. Shirika lenye makao yake nchini Marekani, linaloshughulikia kutoa huduma za afya na tiba-UOSSM na ambalo linaendesha shughuli zake kaskazini magharibi mwa Syria linasema zaidi ya raia 730 wameuliwa na vikosi vya serikali au washirika wao wa Urusi tangu opereshini dhidi ya waasi zilipoanza mwezi Appril uliopita.
China yaonya dhiddi ya kuibuka upya IS
Mjumbe maalum wa China Xie Xiaoyan ameonya akisema kuna kitisho cha kuibuka upya wanamgambo wa itikadi kali wanaojiita "Dola la Kiislam-IS nchini Syria na kuhimiza yafikiwe maendeleo katika utaratibu wa kisiasa kati ya serikali ya rais Bashar al Assad na upande wa upinzani. Mjumbe huyo maalum wa China amesema hayo baada ya kuzungumza na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Geir Pedersen mjini Geneva.
Chanzo: (Reuters/AP)