Wabeba silaha waua 3, wawateka 20 chuoni Nigeria
16 Agosti 2021Tukio hili ni muendelezo wa wimbi la utekaji nyara wa watu wengi unaoendelea kufanywa na makundi ya wabeba silaha chini humo.
Katika ripoti iliyotolewa leo, chuo cha Kilimo na sayansi ya wanyama cha Bakura kupitia msajili wa wanafunzi Aminu Khalid Maradun kimesema kuwa jana Jumapili watu wenye silaha walikivamia majira ya saa nne usiku. Walimuuwa polisi mmoja na maafisa wawili wa usalama, kisha wakawateka watu 20 wakiwemo wanafunzi 15.
Watano kati ya waliotekwa ni wafanyakazi wa chuo hicho na wanafamilia. Wabeba silaha walifanikiwa kuvamia chuo hicho kupitia geti la watembea kwa miguu na kuwachukua mateka. Mapema Jumatatu watekaji hao walipiga simu chuoni hapo wakithibitisha kuwa wanawashikilia mateka 20. Polisi na maafisa wa serikali wa jimbo la Zamfara hawakupatikana kwa haraka kuzungumzia tukio hilo.
Taarifa za makundi yanayoteka watu nyara yakitaka yalipwe fedha zimekuwa zikisikika karibu kila siku katika taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika la Nigeria ikiwa ni miaka saba baada ya kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la Boko Haram lilipoushangaza ulimwengu kwa kuwateka takribani wasichana wa shule 276 kutoka Chibok.
Shule zinazolengwa na magenge ya wahalifu kaskazini na katikati mwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika mara nyingi ni zile zilizo katika maeneo ya mbali ambako wanafunzi hukaa kwenye mabweni wakiwa na walinzi pekee kwa ajili ya usalama wao.
Wanafunzi 950 wametekwa tangu Desemba 2020
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu wanafunzi 950 wametekwa nyara Nigeria tangu mwezi Desemba mwaka uliopita. Wengi wao wameachiliwa huru baada ya kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali katika maeneo husika ingawa wengine bado wanaendelea kushikiliwa.
Wanajeshi wa kulinda usalama pamoja na makubaliano ya amani yamekwama kumaliza machafuko yanayosababishwa na makundi hayo ambayo hujificha katika kambi kwenye msitu wa Rugu unaozunguka majimbo ya Katsina, Kaduna, Zamfara na majimbo mengine ya Niger yakiendela kufanya mashambulizi.