Wabunge Marekani wataka Trump ashtakiwe
20 Desemba 2022Kamati teule ya baraza la wawakilishi imependekeza kutolewa hati ya kushtakiwa dhidi ya Trump, pamoja na kufunguliwa mashtaka mengine ya kuzuwia mchakato rasmi na njama ya kuifanyia udanganyifu Marekani, baada ya uchunguzi uliodumu kwa miazi 18 kuhusu uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Trump katika majengo ya bunge Januari 6, 2021.
Soma pia: Trump atangaza kuwania urais 2024
Watu wasiopungua watano walikufa baada ya kundi la wafanya fujo lililochochewa na madai ya uongo ya Trump kuhusu wizi wa uchaguzi, na kuelekezwa kuandamana hadi bungeni na rais huyo alieshindwa, kuvamia na kupora makao hayo ya demokrasia ya Marekani katika jaribio lililoshindwa la kuzuwia uhamishaji wa madaraka kwa Rais Joe Biden.
Kamati hiyo inayoundwa na wabunge wa vyama vyote ilipiga kura kwa kauli moja kupeleka mashtaka hayo kwa wizara ya Sheria baada ya ufunguzi wa hotuba ya makamu mwenyekiti Liz Cheney ambamo alimshutumu Trump kwa "kukiuka wajibu wa wazi" kwa kushindwa kujaribu mara moja kusitisha ghasia na kumtaja kuwa mtu asiestahiki kushika wadhifa wowote.
"Kila rais katika historia yetu ametetea uhamishaji huu wa amani wa madaraka isipokuwa mmoja. Januari 6, 2021 ilikuwa mara ya kwanza kwa rais mmoja wa Marekani kukataa wajibu wake wa kikatiba wa kuhamisha madaraka kwa amani kwenda kwa mwingine. Katika kazi yetu katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, kamati teule imetambua wajibu wetu wa kufanya kila tuwezalo ili kuhakikisha hili halitokei tena," alisema Cheney.
Soma pia: Trump afunguwa mashitaka kupinga kuitwa mbele ya kamati ya Congress
Rufaa hizo zinaonekana kuwa za kiishara zaidi, kwa kuwa kamati hiyo haina udhibiti wa maamuzi ya mashtaka, ambayo yapo kwa wizara ya sheria. Jack Smith, mwendesha mashtaka maalum huru aliyeteuliwa na Mwanasheria Mkuu Merrick Garland, anaongoza uchunguzi wake binafsi kuhusu Trump kuhusiana na uchaguzi wa 2020.
Trump apinga mashtaka dhidi yake
Trump alitoa taarifa akidai kuwa madhumuni ya uchunguzi huo ni "kunizuia kugombea urais kwa sababu wanajua nitashinda" na kwamba mashtaka yoyote yatakuwa jaribio la "kichama kuniweka kando."
Hatua hiyo ya wabunge ni ya kihistoria, kwa kuwa bunge halijawahi kupendekeza mashtaka ya jinai dhidi ya rais alieko madarakani au wa zamani, na itaongeza kelele miongoni mwa wapinzani wa Trump kutaka kufunguliwa mashtaka.
Pia ni pigo kubwa kwa Trump katikati mwa msururu wa makosa katika wiki kadhaa tangu atangaze nia yake kurejea ikulu ya White House -- ikiwemo matokeo mabaya ya uchaguzi wa katikati ya muhula kwa chama cha Republican katika majimbo ambayo tajiri huyo aliidhinisha wagombea.
Soma pia: Trump na washirika wake huenda walitenda uhalifu
Mashtaka hayo yanaweza kusababisha marufuku ya kushika wadhifa wowote wa umma kwa Mrepublican huyo mwenye umri wa miaka 76, ambaye bado anahodhi mamlaka makubwa ndani ya chama cha Republican, na hata kifungo cha gerezani.
Chanzo: Mashirika