Wabunge Msumbiji kuapishwa leo huku upinzani ukisusia vikao
13 Januari 2025Vyama viwili vya upinzani, vya Renamo na MDM, vimetangaza kususia kikao cha leo Jumatatu, ambacho kitawaapisha wabunge wapya. Chama cha Renamo kilishinda viti 28 katika bunge hilo lenye viti 250 na kile cha MDM kilipata viti vinane.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane amewataka wafuasi wake kufanya maandamano ya amani kuanzia hii leo Jumatatu hadi siku ya Jumatano, wakati Daniel Chapo atakapoapishwa kuwa rais wa Msumbiji.
Mondlane, aliyeungwa mkono na muungano wa Podemos kwenye kura hiyo, amedai alipata asilimia 53 ya kura katika uchaguzi wa rais. Matokeo rasmi yanaonesha alipata asilimia 24 huku mshindi Daniel Chapo akiwa amepata asilimia 65.
Soma pia:Kiongozi wa upinzani Msumbiji aitisha maandamano kwa siku tatu
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane Alirejea nchini Msumbiji kutoka uhamishoni Alhamisi iliyopita kwa lengo la kushinikiza madai yake kwamba alishinda urais.
Amedai kwamba matokeo ya kura ya Rais yalivurugwa na kukipendelea chama cha FRELIMO cha rais mteule Daniel Chapo ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 50 sasa.