Wabunge nchini Uingereza wamuangusha tena Boris Johnson
5 Septemba 2019Wabunge wa Uingereza jana walipiga kura kuunga mkono muswaada wa sheria ya kuizuia Uingereza kujiondowa Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano mwishoni mwa mwezi Oktoba.Hatua ya wabunge imedhihirisha kwamba mkakati wa waziri mkuu Boris Johnson wa kutaka uchaguzi mkuu wa kabla ya wakati umegonga mwamba.
Wabunge kwa mara nyingine wamempa pigo kubwa waziri mkuu Boris Johnson baada ya kuamua kuunga mkono muswada unaoilazimisha Uingereza kutojitowa katika Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano Oktoba 31 na badala yake sasa nchi hiyo inaamanisha itabidi irefushe mchakato wa Brexit hadi Januari 31 mwaka 2020 ikiwa hakuna makubaliano mapya yatakayoidhinishwa na bunge pamoja na Umoja wa Ulaya kufikia Oktoba 19.
Wabunge 327 waliuunga mkono muswaada unaokwenda kinyume na matakwa ya Boris Johnson na 299 walisimama kuupinga. Kwa maneno mengine Boris Johnson ameshindwa kupata wingi wa thuluthi mbili za kumuwezesha kuitisha uchaguzi wa mapema na sasa Muswaada huo utapelekwa mbele ya baraza kuu la wajumbe kabla ya kuwa sheria na kuidhinishwa na Malkia.
Ni mara ya tatu kushindwa bungeni waziri mkuu huyo ndani ya siku mbili lakini anasema wabunge wamefanya kosa kubwa.
''Ni muswaada ambao bila shaka umeshayafikisha mwisho majadiliano,muswaada ambao ni wazi unarefusha muda wa kujitowa umoja wa Ulaya mpaka mwakani au pengine baada ya miaka mingi ijayo,na pia ni muswaada unaoifanya Uingereza kuwajibika kufuata kinachoamrishwa na Brussels,na kuwapa washirika wetu udhibiti.Lakini pia ni muswaada ulioundwa kuyapindua maamuzi ya kidemokrasia ya wananchi katika kura ya maoni iliyopigwa 2016.''
Nje ya bunge la Uingereza wananchi wanaounga mkono nchi yao ibakie kwenye Umoja wa Ulaya walipiga kambi na punde baada ya matokeo ya kura kutangazwa kila mmoja alikuwa na lake la kusema Cliff Dartnaw yeye alisema hivi
''Nataraji Boris Johnson amejionesha jinsi alivyokuwa ni mwanasiasa asiyekuwa na lake jambo anajaribu kuipeleka nchi hii katika mkondo mbaya kabisa.''
Sasa waziri mkuu Johnson anatafuta njia nyingine mpya za kufanikisha uchaguzi wa mapema ufanyike na ofisi yake imeshasema kwamba kiongozi huyo atawageuka wananchi kutafuta uungwaji mkono wa mkakati wake huo wa kutaka uchaguzi ufanyike wiki kadhaa zijazo.
Imesikika kutoka Downing Street kwamba Johnson anataka leo leo kuzungumza moja kwa moja na umma wa Uingereza ingawa maelezo ya kina juu ya hotuba au mkutano anaopanga kuufanya hayajatolewa.Umoja wa Ulaya unawasiwasi na msimamo wa Boris Johnson.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Daniel Gakuba