Wabunge wa Marekani wataka vikwazo dhidi ya Myanmar
19 Oktoba 2017Taarifa hiyo iliyotolewwa kwa pamoja baina ya mshauri wa Umoja wa Mataifa katika kuzuwia mauaji ya maangamizi, Adama Dieng, na mshauri maalum juu ya wajibu wa kulinda, Ivan Simonovic, inasema pia kwamba hata jumuiya ya kimataifa nayo imeshindwa kwenye suala hili la Warohingya.
"Licha ya sisi na maafisa wengine wengi kuonya, serikali ya Myanmar imeshindwa kutimiza wajibu wake chini ya sheria za kimataifa na jukumu la kimsingi la kuwalinda Warohingya dhidi ya mateso," inasema taarifa hiyo.
Lakini wakati washauri hawa wa Umoja wa Mataifa wakitaka hatua kali zichukuliwe na pande husika za mzozo huu, imefahamika kuwa hata huo Umoja wa Mataifa wenyewe haujaamua ikiwa ghasia zinazoendelea dhidi ya Warohingya nchini Myanmar zinaweza kuwekwa kwenye kundi la mauaji ya maangamizi.
Jyoti Sanghera, mkuu wa Ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binaadamu kwa Asia na Pasifiki, ameuambia mkutano kuhusu mauaji hayo hapo jana, kuwa hadi sasa kilichosemwa pekee na Mkuu wa Kamisheni hiyo, Zeid Ra'ad al-Hussein, ni kwamba kinachotokea ni mfano wa kitabuni wa safisha safisha ya kikabila, lakini hajatumia neno mauaji ya maangamizi.
"Bado tunaangalia kwenye mipaka ya kisheria ya jambo hili. Kwa hivyo, kwa sasa limeelezewa kwamba linaokeana kama mfano wa yaliyoandikwa kwenye vitabu kuhusu mauaji ya makusudi dhidi ya kundi fulani la watu. Yanaweza kufika kiwango hicho, lakini bado kwenye Ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa hatujaamua kuita hivyo kisheria," alisema Sanghera.
Wabunge wa Marekani wataka vikwazo dhidi ya Myanmar
Hayo yanajiri wakati wabunge 40 wa Marekani wakiutaka utawala wa Trump kuweka vikwazo vya kusafiri dhidi ya viongozi wa kijeshi wa Myanmar na wote wanaohusika na ukandamizaji dhidi ya Warohingya.
Katika barua yao kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Rex Tillerson, wabunge hao kutoka vyama vyote viwili vya Republican na Democrat, wametaka kile walichokiita "hatua za maana" kwa wote wanaohusika na uvunjwaji wa haki za binaadamu katika operesheni iliyowalazimisha zaidi ya Warohingya 500,000 kuikimbia nchi yao.
"Serikali ya Myanmar inaonekana kukana kinachotokea. Tunataka ufanye kila kiwezekanacho kuhakikisha ulinzi na usalama wa waliokwama ndani ya Myanmar au wale wanaotaka kurejea, na pia kupinga kuwalazimisha kurejea kutoka mataifa jirani," inasema sehemu ya barua hiyo kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Timu ya Umoja wa Mataifa ilikusanya ushahidi kutoka kwa wakimbizi mwezi uliopita, na kwa sasa ujumbe mwengine wa haki za binaadamu uko kwenye eneo hilo kukusanya ushahidi kutoka kwa baadhi ya Warohingya 582,000 waliokimbilia Bangladesh ndani ya kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Wakimbizi hao wameelezea mateso kadhaa yanayojumuisha kufungiwa kwenye makambi, kubakwa na kuharibiwa kabisa kwa vijiji vyao na kulengwa kwa viongozi wa kidini na kitamaduni.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga