1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Marekani wauidhinisha ushindi wa Joe Biden

7 Januari 2021

Baada ya vurugu kutokea kwenye majengo ya bunge mjini Washington, hatimaye Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti yameidhinisha ushindi wa Joe Biden na Kamala Harris kama rais makamu wa rais wa Marekani.

https://p.dw.com/p/3nctF
US-Wahl Kongress | Zertifizierung des Wahlergebnisses
Picha: Erin Schaff/New York Times/AP/picture alliance

Mchakato wa kuthibitisha ushindi huo katika kikao cha pamoja cha mabaraza hayo ulivurugwa jana mchana na kundi la wafuasi wa rais anayeondoka madarakani, Donald Trump ambao waliyavamia majengo ya bunge.

Hatua ya kuidhinishwa kwa kawaida huwa ni utaratibu wa haraka na ni hatua ya mwisho ya kuthibitisha uchaguzi wa urais kwa mujibu wa Katiba ya Marekani. Jumla ya matokeo rasmi ya kura za wajumbe ni 538, ambapo Biden amepata kura 306 na Trump 232.

soma zaidi: Maoni: Siku za mwisho za Trump zimegubikwa na ghasia

Akitangaza matokeo hayo, Amy Klobuchar, Seneta wa Minnesota kupitia chama cha Democratic, ambaye alikuwa miongoni wa waliosimamia mchakato mzima wa kura amesema demokrasia itashinda.

''Rekodi tunayoiweka hapa ni kwamba Joe Biden na Kamala Harris watakuwa rais na makamu wa rais kulingana na kura ambazo tumepewa.'' alisema Klobuchar

Baada ya kuanza tena kwa kikao hicho, kiongozi wa wengi kwenye Baraza la Seneti, Mitch McConnel alilaani ghasia hizo na amesema waliojaribu kuivuruga demokrasia wameshindwa.

Mchakato wa kumuidhinisha Biden wakumbwa na ghasia

USA Washington | Sturm auf das Kapitol
Maafisa wa usalama Marekani wakijaribu kuwaondoa wafuasi wa Trump waliovamia maeneo ya bunge Picha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, mchakato wa kuidhinisha ushindi wa Biden ulikumbwa na ucheleweshaji wa muda mrefu, kutokana na vizingiti vilivyowekwa na wanachama wa Republican kutaka kuhesabiwa upya kura kwenye majimbo ambayo Biden alishinda, ingawa madai hayo yalitupiliwa mbali.

Baada ya ushindi wa Biden kuidhinishwa rasmi na Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti, Rais Trump amesema kutakuwa na ''kipindi cha mpito kilichoratibiwa'' mnamo Januari 20.

Katika ujumbe uliochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter wa Dan Scavino, ambaye ni mkurugenzi wa habari wa Trump, rais huyo wa Marekani amesema ingawa hakubaliani kabisa na matokeo ya uchaguzi, kutakuwa na utaratibu ulioandaliwa wa kukabidhi madaraka. Mtandao wa Twitter umeifunga akaunti binafsi ya Trump baada ya ghasia za jana.

soma zaidi: Wafuasi wa Trump wavamia bunge, dunia yaduwaa

Viongozi mbalimbali duniani wameendelea kuzungumzia tukio hilo la uvamizi wa majengo ya bunge, huku Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel akisema amesikitishwa na vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Trump na kwamba rais huyo wa Marekani anapaswa kulaumiwa kutokana na ghasia hizo.

Merkel amesema anashangazwa na hatua ya Trump kukataa kushindwa katika uchaguzi wa urais wa Novemba 03 uliompa ushindi Biden.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesema uvamizi katika majengo ya bunge la Marekani ni aibu na unapaswa kulaaniwa. Netanyahu amesema hana shaka kwamba demokrasia ya Marekani itashinda.

Chanzo: DPA, AP, AFP, Reuters, DW https://bit.ly/2MBkEs9