1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Uingereza waamua hakuna uchaguzi wa mapema

Sylvia Mwehozi
5 Septemba 2019

Wabunge wa Uingereza wamekataa pendekezo la waziri mkuu Boris Johnson la kuitisha uchaguzi wa mapema mnamo Oktoba 15. Ni pigo jingine kwa waziri huyo mpya anayejaribu kuiondoa nchi yake Umoja wa Ulaya Oktoba 31.

https://p.dw.com/p/3P1be
Brexit - Debatte im Unterhaus
Picha: picture-alliance/dpa/AP/House of Commons/J. Taylor

Katika kura iliyopigwa jana usiku, wabunge hao walikataa pia hoja ya Johnson ya kuiruhusu Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano mwezi ujao. Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Jeremy Corbyn, katika siku za nyuma alitaka uchaguzi mpya ufanyike, lakini chama chake kilijizuia katika kura ya Jumatano. Corbyn Amesema ataunga mkono uchaguzi mpya endapo tu uwezekano wa kuondoka bila ya makubalino utaondolewa. Wabunge wa upinzani wakiungwa mkono na wabunge waasi wa Conservative wanaonya kwamba Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano, kunaweza kusababisha madhara ya kiuchumi yasiyoweza kuzuilika. Johnson alisistiza siku ya Jumatano kwamba mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusu makubaliano mapya, yamepiga hatua lakini muungano huo unasema hakuna mapendekezo mapya yaliyowasilishwa.