Wabunge wa Uingereza wachagua kurefusha Brexit
15 Machi 2019Katika mkwamo kuhusu Brexit , wanasiasa wa Uingereza wamechagua kuuchelewesha. Baada ya wiki za mkwamo wa kisiasa, bunge la Uingereza jana lilipiga kura kutafuta kuahirisha kuondoka kwa nchi hiyo kutoka Umoja wa Ulaya , hatua ambayo huenda ikaepusha kujitoa katika hali ya mvurugiko katika muda uliopangwa wa kujitoa tarehe 29 Machi.
Wakati hatua ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit ikibakia siku 15 na hakuna makubaliano ya kuvunja ndoa ambayo yameidhinishwa hadi sasa, baraza la wawakilishi lilipiga kura 413 dhidi ya 202 kuliomba kundi la mataifa ya Umoja wa Ulaya kuahirisha hatua ya kujitoa hadi Juni 30. Matokeo rasmi yalitangazwa hapo awali kama 412 kwa 202, lakini baadaye yalibadilishwa na kuwa 413 katika orodha rasmi ya upigaji kura.
Kura hiyo inampa waziri mkuu Theresa May muda wa kupumua kidogo, lakini bado ni kipigo cha kiongozi ambaye ametumia miaka miwili akiwaeleza Waingereza kwamba wanajitoa kutoka Umoja wa Ulaya hapo Machi 29.
Hatima ya Uingereza sasa mikononi mwa EU
Nguvu za kuidhinisha ama kukataa kurefushwa kwa hatua hiyo imo mikononi mwa Umoja wa Ulaya, ambao umeashiria kwamba utaruhusu ucheleweshaji pale tu Uingereza ama inaidhinisha makubaliano ya kuachana ama inafanya mabadiliko katika kulishughulikia suala la Brexit.
Katika kichekesho cha kihistoria , karibu miaka mitatu baada ya Uingereza kupiga kura kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya , hali yake ya baadaye hivi sasa imo katika mikono ya kundi hilo la mataifa.
May anatarajiwa kuwaomba viongozi wa Umoja wa Ulaya kurefusha muda wa kujitoa katika mkutano wa viongozi hao hapo Machi 21 hadi 22 mjini Brussels.
Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imesema kuwa Umoja huo utatafakari ombi lolote, "ikitiliwa maanani sababu za na kipindi cha uwezekano wa kurefushwa."
May amelazimika kutafakari uchelewesho wa Brexit baada ya wabunge mara mbili kukataa makubaliano yake ya kuachana na Umoja wa Ulaya na pia kuondoa uwezekano, kimsingi, kujitoa kutoka katika kundi hilo la mataifa bila makubaliano. Kujitoa bila ya makubaliano kutakuwa na maana mparaganyiko mkubwa kwa upande wa makampuni na biashara pamoja na watu nchini Uingereza na mataifa 27 yanayobakia katika Umoja huo.