Wabunge wa Uingereza wapinga mapendekezo mbadala ya Brexit
28 Machi 2019Wabunge wa Uingereza walipiga kura Jumatano usiku juu ya njia mbadala zitakazoweza kutumika kuutatua mkwamo katika mpango wa Brexit. Njia hizo mbadala ni pamoja na:
*Kuondoka Umoja wa Ulaya bila mkataba.
*Kubakia katika umoja wa forodha na soko la pamoja la jumuia hiyo.
*Kuitisha kura ya maoni juu ya mkataba wowote utakaofikiwa.
*Au kuubatilisha mchakato mzima wa Brexit kama hakuna matarajio ya kufikia makubaliano.
Waziri Mkuu Theresa May mapema, alisema angejiuzulu ikiwa mpango wake wa Brexit utapitishwa na wabunge. Akizungumza kwenye mkutano wa chama chake cha Kihafidhina, May aliwaambia wabunge kwamba atajiuzulu kabla ya hatua ya pili ya mazungumzo kuanza.
Hatua hiyo ya kushangaza ya Waziri Mkuu May ni jitihada za mwisho za kutafuta washirika wa kutosha ili kuunga mkono mpango wake mpya anaotarajia kuuwasilisha bungeni kwa mara ya tatu baada ya kukataliwa mara mbili.
Waziri Mkuu May anakabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutoka kwa wabunge wanaounga mkono mchakato wa Brexit katika chama chake cha Kihafidhina wanao mtaka aachie madaraka. Analaumiwa kwa kujadili mpango mbovu wa Brexit utakaoifanya Uingereza inase kwenye Umoja wa Ulaya hata baada ya kuondoka.
Waziri wa mambo ya nje wa zamani Boris Johnson mara moja alitangaza kuwa safari hii atauunga mkono mpango Waziri Mkuu ambao hapo awali aliuita ni wa kudhalilisha. Upo uwezekano mkubwa kuwa Boris Johnson ndiye atakayechukua mahala pa Theresa May kama Waziri Mkuu.
Wakati huo huo chama cha Democratic Union (DUP) cha Ireland ya Kaskazini kinachoiwezesha serikali ya bibi May kuwa na viti vingi bungeni kimesema wazi kwamba kitaupinga mpango wa Waziri Mkuu huyo. DUP imesema mpango huo ni hatari kwa umoja kati ya Ireland na majimbo mengine ya Uingereza.
Matokeo ya jana yanaweza kuifanya Uingereza iendelee kunasa kiuchumi katika Umoja wa Ulaya hatua ambayo itailazimu nchi hiyo iombe muda zaidi kabla ya kujiondoa. Hilo litamaanisha kushiriki kwa Uingereza katika uchaguzi wa bunge la Ulaya utakaofanyika tarehe 23 hadi 26 Mei.
Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya katika suala la Brexit Michel Barnier atakutana leo hii na wajumbe kutoka nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Wajumbe hao watajadili hatua zifuatazo baada ya wabunge wa Uingereza kupiga kura hapo jana.
Naye Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amesema Umoja huo unapaswa kuiruhusu Uingereza kushiriki kwenye uchaguzi wa bunge la Ulaya ikiwa itaashiria kwamba itabadili mchakato wa kujiondoa. Amesisaitiza kwamba Umoja wa Ulaya hautawasaliti mamilioni ya Waingereza ambao wanataka kubakia kwenye jumuia hiyo.
Vyanzo:/APE/RTRE/p.dw.com/p/3Fkfh