Wabunge wa upinzani Uganda wafungwa jela kabla ya maandamano
23 Julai 2024Hatua hiyo ilijiri siku mbili baada ya Rais Yoweri Museveni, ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa karibu miongo minne, kuonya kuwa Waganda wanaopanga kuandamana mitaani leo wanacheza na moto. Msemaji wa polisi ya Uganda Kituuma Ruspke amesema wabunge hao watatu na watu wengine saba walifikishwa mahakamani jana, na kushitakiwa kwa makosa mbalimbali kuwekwa jela.
Soma pia: Upinzani wakaidi marufuku kufanya mikutano ya kisiasa kutoka kwa polisi
Hakutoa maelezo zaidi kuhusu mashitaka yao lakini msemaji wa NUP Joel Ssenyonyi alisema wabunge hao walishitakiwa kwa kukiuka sheria za barabarani na kuwazuia maafisa wa polisi, mashitaka ambayo wanayakanusha. Wabunge hao ni Francis Zaake, Charles Tebandeke na Hassan Kirumira, wote wa chama cha upinzani cha National Unity Platform - NUP na watafikishwa mahakamani Alhamisi kwa ajili ya kusikilizwa shauri lao la kuwachiwa kwa dhamana.
Hayo yanajiri wakati waandamanaji wakiapa kuendelea na maandamano yao ya kupinga ufisadi, wakihimizwa na maandamano ya kuipinga serikali yanayotarajiwa kuendelea leo katika nchi jirani Kenya. Kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alisema kuwa vikosi vya usalama viliyazingira makao makuu ya chamachake Jumatatu.