1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wausasambua mpango wa brexcit wa Boris Johnson

3 Oktoba 2019

Mpango mpya wa waziri mkuu Boris Johnson umewasilishwa bungeni na kukosolewa na wabunge kutoka vyama takriban vyote nchini Uingereza baada ya Umoja wa Ulaya pia kuonesha kutoridhishwa kabisa na mpango huo.

https://p.dw.com/p/3Qh4X
Großbritannien London | Wiederaufnahme der Parlamentssitzung - Boris Johnson
Picha: Reuters/Parliament TV

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amewasilisha bungeni mjini London mapendekezo yake mapya kuhusu Brexit, baada ya hapo jana kuyawasilisha mapendekezo hayo mbele ya viongozi wa Umoja wa Ulaya. Hata hivyo mapendekezo hayo yameibua mabishano makali ndani ya bunge la Uingereza.

Mjadala mkali umeibuka bungeni Westminster huko London baada ya wabunge kukabidhiwa mpango mpya wa Boris Johnson na kuujadili. Kundi muhimu la wabunge wa Umoja wa Ulaya limesema bunge la Ulaya halikuweza kuunga mkono makubaliano kwa kuzingatia mapendekezo hayo mapya ya Uingereza ambayo hayajafikia vigezo vinavyotakiwa kuhusu suala la mpaka.

Ndani ya bunge la Uingereza kiongozi wa chama kinachotawala Scotland cha SNP Ian Blackford amesema mapendekezo ya sasa ya waziri mkuu Boris Johnson hayakubaliki mbele ya Wascotland.

'' Mapendekezo haya hayakubaliki, hayawezi kufanyiwa kazi, hayawezi kupendekezwa. Yanahusu tu kumbebesha lawama mtu mwingine, na kwa maana hii katika Umoja wa Ulaya mpango huu umekataliwa. Bwana spika mpango huu umetengenezwa kushindwa na hilo analijuwa waziri mkuu. Hiki kitiisho cha kuwataka watu waukubali au wauachilie mbali ni shinikizo jingine linalotueleza kwenye hatua ya kuondoka Umoja wa Ulaya kwa janga kubwa.''

Ian Blackford pia amesema wabunge wa Scotland wako tayari kuiangusha serikali ya Boris Johnson ikiwa waziri mkuu huyo atashikilia msimamo wa kulazimisha Brexit bila makubaliano.

Großbritannien London | Wiederaufnahme der Parlamentssitzung
Picha: picture-alliance/AP Photo/House of Commons/J. Taylor

''Namwambia waziri mkuu, tafuta njia urefushe muda wa Brexit  au ujiuzulu, la sivvyo SNP iko tayari kuiangusha serikali hii.''

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Jeremy Corbyn amesema hakuna mbunge yoyote wa chama chake atakayeunga mkono mapendekezuo mapya ya waziri mkuu Boris Johnson ambayo amemesema hayana tafauti na yale yaliyokataliwa huko nyuma.

Mbunge wa chama cha Labour Hilary Benn kwa upande wake amesema mapendekezo ya Johnson yanayojumuisha vituo vya ukaguzi wa mizigo Ireland ya Kaskazini, unahatarisha kurudisha hali iliyokuwa mwanzo ya masharti makali ya mpaka.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Ireland Leo Varadkar amesema huenda wakalazimika kukubaliana na hatua ya kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano kwa kipindi cha muda fulani ikiwa hakuna mwafaka utakaopatikana juu ya suala hili la Brexit na Umoja wa Ulaya. Lakini waziri mkuu huyo amesema hawezi kutabiri matokeo ya mazungumzo ya Brexit lakini angependelea kuona makubaliano yanafikiwa na Uingereza inajitowa kwa njia ya kistaarabu.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW