1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachezaji 2 wa Dynamo Dresden wana COVID-19

Josephat Charo
9 Mei 2020

Wachezaji wawili wa klabu ya ligi ya daraja la pili ya Bundesliga Dynamo Dresden Ijumaa (08.05.2020) wamepatikana na ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3bzJZ
Fußball mit dem Logo des Fußball-Zweitligisten SG Dynamo Dresden
Picha: picture-alliance/dpa/R. Michael

Dresden, ambayo inaburuza mkia katika ligi ya daraja la pili, ilipangiwa kukwaana na Hannover ugenini Mei 17 wakati ligi itakaporejea tena baada ya kusimamishwa kwa miezi miwili, lakini kikosi kizima, makocha na wasimamizi lazima wakae karantini nyumbani kwa siku 14.

"Tunawasiliana na maafisa husika wa afya na bodi ya ligi kuratibu hatua zote zitakazofuata. Ukweli ni kwamba hatuwezi kufanya mazoezi wala kushiriki mechi yoyote katika kipindi cha siku 14 zijazo," mkurugenzi wa michezo wa Dynamo Dresden, Ralf Minge, alisema.

Wachezaji hawajatambuliwa. Matokeo yao yaligunduliwa katika awamu ya tatu ya upimaji uliofanywa katika klabu hiyo Ijumaa kama sehemu ya utaratibu wa bodi ya ligi, DFL, kuhakikisha soka linarejea viwanjani Ujerumani.

Mchezaji mmoja aligunduliwa na COVID 19 katika wimbi la kwanza la upimaji wikendi iliyopita. Amekuwa katika karantini tangu Mei 4. Timu ilirejea katika mazoezi kamili siku ya Alhamisi.

Kansela Angela Merkel alikuwa ametangaza siku moja kabla kwamba ligi kuu na ligi ya daraja la pili zingeanza tena Mei 16 bila mashabiki viwanjani. Timu zilitakiwa kufanya mazoezi zikiwa zimejitenga kabla mechi kuanza.

Dynamo Desden inasema wachezaji wake wawili waliopatikana na COVID 19 Ijumaa hawakuonesha na bado hawaoneshi dalili zozote za virusi vya corona.

(ap)