Wadukuzi wazishambulia tovuti za serikali Myanmar
18 Februari 2021Kundi moja la wadukuzi wa Myanmar leo walidukua tovuti kadhaa za serikali ikiwemo ile ya benki kuu, tovuti ya bandari na ya mamlaka ya chakula na dawa, kulingana na taarifa ya televisheni ya taifa ya MRTV.
Wadukuzi hao waliandika kupitia ukurasa wa Facebook kwamba "wanapigania haki nchini Myanmar", na kwamba kitendo hicho ni sawa na maandamano makubwa ya watu mbele ya tovuti za serikali. Gazeti la serikali la New Light nalo lilithibitisha taarifa za kuvamiwa tovuti ya jeshi.
Hayo yakijiri, mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar Tom Andrews ameonya juu ya kutokea ghasia kubwa wakati waandamanaji wakisonga mbele na maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi. Mjumbe huyo amesema amepokea ripoti za kusambazwa wanajeshi katika mji mkubwa wa Yangon.
"Ninamaanisha watu wa Myanmar wanaelewa kitu wanachoweza kufanya jeshi na majenerali , wameshuhudia. Na hivyo uwepo wa jeshi, vikosi vyao na ongezeko la uwepo wa wanajeshi na wapi wanajeshi hawa wanatokea, ni kitu kinachonipa wasiwasi."
Maandamano ya nchi nzima yameendelea tena leo licha ya hofu iliyotanda usiku mzima kwenye mji mkubwa wa pili wa Mandalay ambako polisi na wanajeshi walivunja maandamano yaliyokuwa yamezuia reli. Maandamano hayo ya kila siku na migomo ambayo imeathiri ofisi nyingi za serikali, hayaonekani kupungua kasi licha ya utawala wa kijeshi kuahidi uchaguzi mpya na kuwaomba watumishi wa umma kurejea kazini, na kutishia kuwachukulia hatua kinyume na hivyo.
Wakati huohuo mawaziri wa mambo ya nje wa Singapore na Indonesia wanaamini kuwa jumuiya ya mataifa ya kusini na mashariki mwa Asia, ASEAN inaweza kuwa na mchango mkubwa wa kuhimiza mazungumzo ya kurejesha amani nchini Myanmar. Kauli yao imetolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Indonesia Retno Marsudi wakati alipokutana na mwenzake wa Singapore Vivian Balakrishnan hii leo.
Kwa pamoja walijadiliana juu ya uwezekano wa hatua za haraka zinazoweza kuchukuliwa na jumuiya ya ASEAN kuelezea hali nchini Myanmar ambako kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia Aung San Suu Kyi aliondolewa mamlakani kwenye mapinduzi ya kijeshi februari mosi.