1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waemirati watakaokosoa kutengwa Qatar waonywa

Jane Nyingi
7 Juni 2017

Umoja wa falme za kiarabu umeonya yeyote atakayeonyesha huruma kutokana na vikwazo ilivyowekewa Qatar na mataifa jirani zake, huenda akatupwa gerezani  hadi miaka 15.

https://p.dw.com/p/2eExK
Katar Die neuen Hochhäuser der Innenstadt von Doha
Picha: Picture alliance/AP Photo/K. Jebreili

Umoja wa falme za kiarabu umeonya yeyote  atakayeonyesha huruma  kutokana na vikwazo ilivyowekewa Qatar na mataifa jirani zake, huenda akatupwa gerezani  hadi miaka 15. Umoja huo, Saudi Arabia,Misri na Bahrain zilikatiza uhusiano wake wa kidiplomasia na Qatar  jumatatu wiki hii na  kuwapa raia wake muda wa siku 14  kuondoka ,kwa shutuma kuwa Doha inaunga mkono ugaidi. Qatar imeyakanusha madai hayo. 

Katika  taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti la  Gulf na Al Bayan, mwanasheria mkuu wa umoja huo wa falme za kiarabu amesema  watakaopatikana na hatia ni pamoja na wale  wanaoshiriki mazungumzo iwe ni hata katika mitandao ya kijamii, kukosoa msimamo iliochukuliwa na umoja huo,pamoja na mataifa  mengine ya kiarabu dhidi ya Qatar.Kando na kifungo cha miaka mitatu hadi miaka 15 gerezani, kutakuwepo pia na faini ya hadi dola 13,660.Umoja huo wa falme za kiarabu, Saudi Arabia,Misri na Baharin pia zilifunga anga zake kwa ndege za Qatar na hata kupiga marufuku kituo cha televisheni kilicho na makao yake makuu nchini Qatar cha al jazeera. Kama yalivyo mataifa mengi ya Ghuba,Umoja wa falme za kiarabu una sheria kali  za kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni na kumharibia mtu jina ambazo hata zimeshtumiwa vikali na makundi  ya kimataifa ya haki za binadamu. 

Katar nach dem Boykott
Watu wafurika maduka ya Doha kutokana na wasiwasi wa kupungua bidhaa muhimuPicha: picture-alliance/AP Photo/Doha News

Ibara ya 29 ya sheria ya uhalifu wa mtandanoni unalifanya kuwa kosa la jinai chapisho lolote la taarifa  kwenye mtandao kwa nia ya kukejeli au kuharibu sifa ya taifa au nembo zake.Wakati huo huo serikali ya Qatar ipo katika mazungumzo na Iran na Uturuki kupata chakula na maji huku kukiwa na wasiwasi wa kutokea uhaba wa mahitaji hayo, baada ya wasambazaji wakuu wa bidhaa hizo, Umoja wa Falme za kiarabu na Saudia kukatiza  hata uhusiano wake wa kibiasahara na Qatar. Mafisa nchini Qatar wamesema wanachakula cha kutosha kwa muda wa hadi wiki nne,na pia  serikali ina ghala kubwa  la kuhifadhi nafaka mjini Doha. Akizungumza mjini Ankara, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameshikilia kuwa kutengwa Qatar  hakutasadia kwa vyovyote“Jambo sahihi la kufanya mataifa  wanachama wa baraza la ushirikiano la Ghuba ni kufanya mazungumzo kuyatatua matatizo yaliyopo. Kwa hali hii tunaishukuri Qatar kwa kusalia tulivu na msimamo wake thabiti. Kwa kujaribu kuitenga Qatar ,ambayo kwa uhakika imekuwa ikijitahidi kukabiliana na ugaidi,hakutachangia kwa vyovyote kuyatatua matatizo yeyote” 

Mauritania pia imetangaza kukatiza uhusiano wake wa kidiplomasia na Qatar na kuifanya nchi ya hivi karibuni zaidi kuchukua hatua hiyo. Katika taarifa iliyotolewa na wizara yake ya mambo ya nje ,taifa hilo la Afrika  limeishtumu Qatar kwa kushirikiana na mashirika ya kigaidi

Mwandishi:Jane Nyingi/AP/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga