Kabuga kwenda the Hague
20 Mei 2020Waendeshamashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wametoa waranti wa kutaka mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Felicien Kabuga, apelekwe katika vizuizi vya Umoja wa Mataifa na kesi yake iendeshwe na mahakama hiyo. Kabuga mwenye umri wa miaka 84 amefikishwa katika mahakama hiyo akisukumwa katika kiti cha magurudumu, huku akiwa kavaa barakoa.
Mtuhumiwa huyo kigogo katika mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyoangamiza maisha ya watu zaidi ya 800,000, amezungumza kuthibitisha utambulisho wake. Kabuga alifikishwa katika mahakama ya rufaa ya mjini Paris katika msafara uliokuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na kesi yake kuanza kusikilizwa saa tatu baadaye, imesema duru ya mahakama hiyo. Alikamatwa mjini Paris Jumamosi iliyopita, baada ya kuukwepa mkono wa sheria kwa zaidi ya miaka 26, akishukiwa kutoa mchango mkubwa katika mauaji hayo yaliyolenga kuangamiza kabisa jamii ya Watutsi nchini Rwanda.
Maandalizi ya kwenda the Hague yameanza.
Tayari waendeshamashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu yenye makao yake mjini The Hague, wamesema wamekwishawasilisha hati za kutaka Kabuga ahamishiwe katika vizuizi vya mahakama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, kama ilivyothibitishwa na Serge Brammertz, mmoja wa waendeshamashtaka hao. Kabuga anaweza kuhamishiwa mjini The Hague, kabla ya kupelekwa Arusha yalipo makao ya chombo cha Umoja wa Mataifa cha kushughulikia kesi za washukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Alishtakiwa rasmi mnamo mwaka 1997 kwa makosa saba ya uhalifu yote yakifunganishwa kwa mauaji hayo mabaya ya mwaka 1994.
Wakati hayo yakijiiri, Kundi linalotoa msaada kwa wahanga wa mauaji ya kimbari ya Rwanda lenye makao nchini Ufaransa "Ibuka France”, limesema linataka uchunguzi kufanyika ili kubaini jinsi Kabuga alivyo weza kujificha ndani ya ardh ya Ufaransa.
Kundi hilo linasema linashuku kuwa Kabuga alikuwa akipata usaidizi zaidi ya ule kutoka kwa familia yake tu. Mkuu wa Ibuka France Etienne Nsanzimana amesema yapo maswali yanayohitaji majibu, kama muda halisi ambao mtuhumiwa huyo aliweza kujificha nchini Ufaransa, na alipopata uwezo wa kuishi kifahari kwa kipindi hicho.
Takriban watu 800,000 wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Watutsi waliuawa ndani ya siku 100 katika mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliotekelezwa na serikali ya Kihutu ikisaidiwa na makundi ya wanamgambo wa kikabila.Kabuga mfanyabiashra wa Kihutu anashtakiwa kufadhili na kuyapa silaha makundi hayo. Hadi kufikia sasa haijulikani jinsi mtuhumiwa huyo ambaye Marekani iliweka zawadi ya kitita cha dola milion 5 kwa atakayewezesha kukamatwa kwake, alivyoweza kuingia nchini Ufaransa.
Chanzo: Reuters