1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi ambao ni mtihani kwa Abiy Ahmed wafanyika Ethiopia

21 Juni 2021

Raia wa Ethiopia wanashiriki uchaguzi wa mabunge ya kitaifa na majimbo katika zoezi ambalo ni mtihani mkubwa kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed huku uchaguzi ukicheleweshwa katika majimbo 100 kati ya 547 nchini humo.

https://p.dw.com/p/3vGzI
Äthiopien Wahl 2021 | Wahllokal Addis Abeba
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Uchaguzi huo uliocheleweshwa tangu mwaka uliopita ni moja ya mageuzi aliyoyaahidi Abiy Ahmed ambaye kuingia kwake madarakani mwaka 2018 kuliashiria kumalizika kwa utawala wa kiimla na kumpelekea kushinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka uliofuata. Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia ameuelezea uchaguzi wa leo kama jaribio la kwanza kwa taifa hilo kuandaa uchaguzi ulio huru na haki.

Misururu mirefu ya wapiga kura waliovalia barakoa ilionekana mji mkuu Addis Ababa huku usalama ukiimarishwa kote katika taifa hilo la pili barani Afrika kwa idadi kubwa ya watu. Magari ya kijeshi pia yalionekana yakiegeshwa katika maeneo kadhaa mjini humo. Zaidi ya raia milioni 37 wa Ethiopia wanashiriki uchaguzi wa leo. 

soma zaidi: Watu wa Ethiopia kupiga kura katika uchaguzi mkuu Jumatatu

Desalgn Shume ni mmoja ya wapiga kura mjini Addis Ababa anasema kile wanachohitaki ni serikali itakayoleta amani, umoja na serikali itakayositisha mauaji yanayoendelea. Na pia raia wa Ethiopia wanahitaji kuokolewa kutoka katika ubaguzi wa kikabila. Wendwosen Dagnaw mkaazi mwengine wa jimbo la Amhara anasema kile anachohitaji ni amani na muungano wa watu wote Ethiopia.

"Mimi natokea jimbo la Amhara nataka nchi yetu iungane na kusonga mbele kwa amani kama taifa. natumai hakutakuwa na mizozano au migogoro katika siku za usoni kama ilivyokuwa awali," aliendelea kusema Wendwosen Dagnaw.

Chama kitakachoshinda wingi wa kura katika bunge la wawakilishi ndio kitakachokuwa na nafasi ya kuunda serikali, na chama tawala cha Prosperity Party chake Abiy Ahmed ndicho kinachotarajiwa kushinda na kuendelea kubakia madarakani.

Upinzani wakishutumu chama tawala kwa nyanyasaji na vitisho dhidi yao

Parlamentswahl in Äthiopien 2021
Wapiga kura wakiwa nje ya kituo cha kupigia kura mjini Ambo, Ethiopia Picha: S. Getu/DW

Hata hivyo upinzani ambao baadhi yao wameususia uchaguzi wa leo hasa katika jimbo la Oromia wamekishutumu chama tawala kwa kile walichokielezea kama unyanyasaji wa serikali na vitisho huku wengine wakisema walinyimwa nafasi ya kushiriki kampeni katika maeneo kadhaa nchini humo.

soma zaidi: Asilimia 90 ya raia wa Tigray wanahitaji msaada wa kiutu

Uchaguzi huu unafanyika wakati Abiy Ahmed aliye na miaka 44 akikosolewa kufuatia mapigano yanayoendelea katika jimbo la Tigray Kaskazini mwa Ethiopia, yalioanza kutokana na kiongozi wa waasi katika eneo hilo kupinga kucheleweshwa kwa uchaguzi kufuatia janga la COVID 19.  Hata hivyo hakuna tarehe yoyote iliyotolewa kwa uchaguzi kuendeleo kufanyika huko pamoja na majimbo mengine 38 ambako uchaguzi umecheleweshwa kufuatia vita na masuala ya usimamizi.

Wasiwasi wa Jumuiya ya kimataifa kuhusu namna uchaguzi utakavyoendeshwa umezidi kuongezeka, Umoja wa Ulaya imekataa kutuma waangalizi katika uchaguzi huyo huku Marekani ikitilia mashaka ya mazingira ya uendeshaji wa uchaguzi huo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa Antonio Guterres ameonya kuhusu matukio ya vurugu lakini serikali ya Ethiopia imesema wasiwasi wa Jumuiya hiyo haiizuwii kuendelea na uchaguzi inaoamini utakuwa wa huru na haki.

Vyanzo: reuters, ap,afp