Wafadhili wakwama kukusanya dola bilioni 10 kuisadia Syria
31 Machi 2021Umoja wa Mataifaulikuwa na matumaini ya kukusanya kiasi cha dola bilioni 10 katika mkutano wa siku mbili uliofanyika kwa njia ya video kwa ajili ya kuwasaidia Wasyria. Janga la virusi vya corona limechangia idadi ya watu wanaohitaji msaada kuongezeka katika mgogoro wa nchi hiyo uliodumu kwa miaka kumi.
Kamishna wa usimamizi wa mizozo wa Umoja wa Ulaya Janez Lenarcic alisema dola bilioni 4.4 zimeahidiwa kutolewa kwa ajili ya mwaka huu wa 2021 na dola bilioni mbili zitatolewa kwa mwaka 2022 na zaidi.
Umoja wa Mataifa ulisema awali kwamba dola bilioni 10 zilizokuwa zikitajika kwa mwaka wa 2021, zilikusudiwa kuwasaidia raia walioko ndani ya Syria na wakimbizi katika mataifa jirani.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema katika mkutano huo kwamba watu zaidi ya milioni 13 wanahitaji usaidizi wa kiutu ili kuweza kuvuka mwaka huu. Kwa ujumla Umoja wa Mataifa unadai kwamba watu milioni 24 wanahitaji kusaidiwa nchini humo na katika ukanda mzima.
Nchi jirani na Syria za Uturuki, Lebanon, Jordan na Iraq zinakabiliwa na matatizo yake binafsi ya kiuchumi na hivyo kushindwa kumudu mzigo wa kuwahudumia wakimbizi.
Ujerumani ambayo ni mfadhili mkuu iliahidi kutoa euro bilioni 1.74 na Marekani dola milioni 600. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas alisema katika mkutano huo kwamba janga la Syria halipaswi kudumu tena kwa miaka mingine 10
"Leo Ujerumani inatoa ahadi yake kubwa zaidi katika miaka minne iliyopita, euro bilioni 1.738. Janga la Syiria halipaswi kudumu kwa miaka mingine 10. Kuumaliza mgogoro huo kunaanza na kurudisha tumaini. Kunaanza na ahadi zetu hapa leo."
Vita nchini Syria vimewaua watu ziaidi ya 388,000 na mamilioni kukosa makaazi. Juhudi za kutafuta amani ya kudumu zimekwama na kusababisha kundi linalojiita dola la kiislamu kuanza kupata nguvu tena.
Mapema siku ya jumatatu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alitoa wito kwa Urusi ambayo ni mshirika muhimu katika mgogoro huo kufungua tena njia ili kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu, wito ambao uliungwa mkono na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell.
Umoja wa Ulaya unasisitiza kwamba hakuwezi kuwepo na usaidizi wa kimataifa wa kuijenga upya Syria bila ya makubaliano ya amani kati ya rais Bashar al Assad na makundi ya waasi na upinzani.