Wafadhili watakiwa kuwekeza Afghanistan
8 Julai 2012Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon , ambaye ni miongoni mwa viongozi maarufu waliokusanyika katika mji mkuu wa Japan Tokyo kwa ajili ya mazungumzo juu ya kile kinachojulikana kama , "muongo wa mabadiliko" amesema kuwa hatua za maendeleo katika usalama na maendeleo kwa jumla zimepigwa, lakini bado ni tete.
Kushindwa kuwekeza katika serikali , sheria, haki za binadamu, ajira na maendeleo ya jamii kunaweza kurejesha nyuma uwekezaji na hatua za kujitolea muhanga ambazo zimefanyika katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Ban amewaambia viongozi katika mkutano huo.
Mkutano huo una lengo la kupunguza mwanya kati ya kile ambacho serikali mjini Kabul inakipata kutokana na uchumi wake na kile inachohitaji kwa ajili ya maendeleo ya nchi hiyo na kuwa thabiti.
Afghanistan yataka msaada
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai, ambaye yuko mjini Tokyo pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon , ametoa wito wa nchi yake kupatiwa kiasi cha dola bilioni 4 kila mwaka kama msaada wa kijamii.
Siku ya Jumamosi Japan ilitangaza kuwa wafadhili watatoa zaidi ya dola bilioni 16 kama msaada wa kijamii katika muda wa miaka minne hadi mwaka 2015.
Tuko katika wakati mgumu katika historia ya Afghanistan, katika hatua za mpito kutoka utegemezi wa misaada ambayo imesaidia taasisi za nchi hiyo kuota mizizi hadi katika uhusiano wa kawaida wa kitaifa, Afghanistan inayoweza kufanyakazi pamoja na watu wake pamoja na washirika wake wa kimataifa, Ban amesema.
Usalama bado tatizo
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo , rais wa Afghanistan Hamid Karzai amekiri kuwa usalama unaendelea kuwa tatizo kubwa, lakini ameongeza kuwa nchi yake imetoka mbali hadi ilipo sasa.
Katika miaka kumi iliyopita , kwa msaada kutoka jumuiya ya kimataifa , tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo kuelekea kuponesha makovu ya mizozo na uharibifu, amesema.
Tunajenga njia mpya kwa ajili ya watu wetu kufikia yale wanayokusudia ya mafanikio ya amani pamoja na kuwa na nchi yenye demokrasia.
Watu walioko ndani na nje ya nchi hiyo wanahofia kuwa mara Marekani pamoja na washirika wao hawatakuwa na shaka tena na maisha ya wanajeshi wao kufariki nchini Afghanistan baada ya kuondoa majeshi hayo mwaka 2014, nchi hiyo inaweza kuachwa kutumbukia katika mikono ya wababe wa kuuza madawa ya kulenywa na makundi yenye imani kali za kidini.
Marekani kuendelea kuisaidia Afghanistan
Serikali ya rais Barack Obama italiomba baraza la Congress kuendeleza msaada wa Marekani kwa Afghanistan karibu na kiwango ilichokuwa ikitoa katika muongo mmoja uliopita hadi mwaka 2017 kama sehemu ya juhudi za kimataifa kuimarisha nchi hiyo hata pale ambapo majeshi ya kimataifa yataondolewa katika muda wa miaka miwili ijayo.
Viongozi kutoka mataifa 80 pamoja na mashirika ya kimataifa waliokusanyika mjini Tokyo, mji mkuu wa Japan , wanatarajiwa kuidhinisha kile kinachojulikana kama , azimio la Tokyo, linalopendekeza kuungwa mkono pamoja na kutoa fedha kwa serikali ya mjini Kabul.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/ ape
Mhariri : Bruce Amani