Wafalme wa soka Uhispania wafunga virago
19 Juni 2014Baada ya kubamizwa magoli matano kwa moja katika mchuano wao wa ufunguzi, Uhispania ilisambaratishwa tena na mara hii mikononi mwa Chile katika uwanja wa Maracana, ambao walifunga magoli mawili katika kipindi cha kwanza kabla ya kuziba lango lao katika kipindi cha pili.
Kichapo hicho kilimfanya nahodha wa Uhispania na mlinda lango Iker Casillas kuomba radhi kwa kila mmoja akisema kuwa wanawajibika kwa matokeo hayo lakini pia akaongeza kuwa wao ndio wa kwanza kuhisi uchungu.
Wafalme hao wa kandanda ulimwenguni katika miaka ya karibuni, Uhispania walishinda Kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka wa 2008 na Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini miaka minne iliyopita pamoja na Kombe la UEFA Euro 2012. Lakini umahiri wao haupo tena na kikosi chao kinachozeeka kinastahili mabadiliko makubwa.
Chile ambao hawajawahi kuwapiku Uhispania katika mechi kumi za awali, walionekana wenye makali zaidi kutoka mwanzo. Eduardo Vargas alimgeuza kipa Casillas ndani ya kijisanduku, akauruka mguu wa beki Sergio Ramos na akabusu wavu katika dakika 20 za mchezo, kabla ya Charles Aranguiz kufunga goli la pili muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kukamilika. Mkufunzi wa Uhispania Vicente del Bosque amewaambia wanahabari baada ya mpambano huo kuwa hawana chochote cha kulalamikia kwa sababu walistahili kubanduliwa nje. Alikiri kuwa Chile waliwazidi maarifa.
Kiungo wa Chile Arturo Vidal, ambaye alionyesha mchezo wa kusisimua, alijigamba akisema kuwa walionyesha kuwa wako katika kiwango kizuri sana. Alisema hawakwenda Brazil katika likizo, bali kuwania ubingwa.
Mashabiki wa Chile wavamia uwanja
Lakini kabla ya kuanza mamia ya mashabiki wa Chile ambao hawakuwa na tikiti za kuingia uwanjani waliingia wka nguvu katika uwanja wa Maracana, huku wakiuvunja ukuta wa eneo moja la uwanja. Maafisa wa BRAZIL pamoja na wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA wamesema mashabiki 85 walikamatwa kutokana na vurumai hizo.
Hiyo ni mara ya pili ambapo mashabiki wameingia kwa nguvu katika uwanja huo wa Maracana mjini Rio de Janeiro wiki hii, tukio ambalo ni kitisho cha usalama katika uwanja utakaoandaa fainali ya dimba hilo mnamo Julai 13. FIFA imekilaani kitendo hicho ikisema mashabiki hao hawakuweza kuingia uwanjani kuangalia mechi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu