1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafaransa kumchagua Rais mpya kati ya Macron na Le Pen

Caro Robi
7 Mei 2017

Wapiga kura nchini Ufaransa leo wanamchagua rais wao mpya kati ya Emmanuel Macron mgombea urais anayefuata siasa za wastani na Marine Le Pen mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia.

https://p.dw.com/p/2cXg9
Frankreich Bildkombo Emmanuel Macron und Marine Le Pen
Picha: AFP/Getty Images

Uchaguzi huo wa Jumapili unakuja baada ya kipindi cha kampeini kilichoshuhudia kashfa, matukio ya kushangaza na dakika za mwisho kampeini za Macron kudukuliwa na nyaraka nyeti kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

Macron mwenye umri wa miaka 39 ambaye awali hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa kuchaguliwa na wananchi ambaye anaunga mkono kuimarika kwa Umoja wa Ulaya anamenyana na Le Pen anayepinga uwepo wa Umoja huo, wahamiaji, sarafu ya euro na kutetea siasa kali za kizalendo.

Le Pen kiongozi wa siasa kali

Le Pen mwenye umri wa miaka 48 amesema uchaguzi huo utakuwa ni kinyang'anyiro kati ya wanaounga mkono soko huru na uhamiaji na wazalendo wanaotetea mipaka thabiti na kuwepo kwa utambulisho wa kitaifa.

Präsidentschaftskandidat Marine Le Pen
Mgombea wa Urais Ufaransa Marine Le PenPicha: Getty Images/J. J. Mitchell

Vituo 66,546 vya kupigia kura vitafunguliwa saa mbili asubuhi asubuhi  na kufungwa saa moja jioni sipokuwa katika miji mikubwa ambapo vitasalia wazi kwa saa moja zaidi. Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa muda mfupi baada ya vituo vya kupiga kura kufungwa.

Zoezi la kupiga kura lilianza jana katika himaya za nje za Ufaransa. Wananchi wa Saint-Pierre na Miquelon, himaya zilizo chini ya Ufaransa katika eneo la Mashariki ya pwani ya Kanada walianza kupiga kura Jumamosi.

Chunguzi za maoni ya wapiga kura zinaonesha Macron mshindi wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais iliyofanyika mwezi uliopita akiongoza kwa umaarufu kwa takriban asilimia 62 dhidi ya Le Pen anayeungwa mkono kwa asilimia 38.

Macron abashiriwa kuwa Rais

Yeyote kati ya wagombea hao wawili atakayeshinda uchaguzi wa Jumapili atasababisha mabadiliko makubwa Ufaransa, taifa la sita duniani lililo imara kiuchumi, mwanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na lenye nguvu za kijeshi.

Präsidentschaftswahl in Frankreich Emmanuel Macron
Mgombea Urais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: picture alliance / Christophe Ena/AP/dpa

Hii ni mara ya kwanza vyama vikuu nchini humo havina mgombea katika duru ya pili ya uchaguzi tangu 1958. Iwapo atashinda, Macron atakuwa Rais mwenye umri mdogo zaidi kuiongoza Ufaransa. Waziri huyo wa zamani wa uchumi ameahidi kupunguza matumizi ya serikali, kulegeza sheria za leba, kuimarisha elimu katika maeneo duni na kuyalinda maslahi ya wajasiriamali. Pia anaunga mkono kuwepo kwa Umoja wa Ulaya thabiti hasa baada ya Uingereza kujiondoa kutoka Umoja huo.

Kwa upande wake Le Pen kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Bational Front ameahidi iwapo atashinda ataitisha kura ya maoni kuiondoa Ufaransa kutoka Umoja wa ulaya, kuondolea mbali matumizi ya sarafu ya euro nchini humo, ameapa kupunguza idadi ya wahamiaji Ufaransa itakuwa ikipokea kwa mwaka, kupunguza umri wa kustaafu na kuanzisha sheria kali za kupambana na kitisho cha itikadi kali za Kiislamu.

Rais mpya atakayechukua hatamu za uongozi kutoka kwa Rais wa sasa Francois Hollande anatarajiwa kuapishwa mnamo tarehe 14 mwezi huu.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Sudi Mnette