1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafaransa waanza kupiga kura ya kumchagua rais mpya

23 Aprili 2017

Raundi ya kwanza ya chaguzi wa rais wa nchini Ufaransa inafanyika leo hii.  Emmanuel Macron aliyekuwa waziri wa uchumi wa nchi  hiyo ndie anayepewa nafasi ya juu ya kushinda.

https://p.dw.com/p/2bkKJ
Frankreich elf Präsidentschaftskandidaten treten in TV-Debatte gegeneinander an
Picha: picture alliance/abaca/J. Domine

Macron mwenye umri wa miaka 39  anautetea Umoja wa Ulaya. Mgombea wa  chama cha  siasa za mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen ambaye ni mpinzani mkubwa wa Umoja wa Ulaya na anayetaka kuiondoa sarafu ya Euro nchini Ufaransa ameahidi kuitisha kura ya maoni ili watu wa Ufaransa wachague iwapo wanataka kujiondoa au kubakia  katika Umoja wa Ulaya.

Wananchi wenye haki ya kupiga kura leo wanapiga kura katika duru ya kwanza ya kumchagua rais mpya . Katika mfumo wa uchaguzi nchini humo rais anachaguliwa baada ya kufanyika duru mbili za uchaguzi.  Wagombea wakuu wanne wanawania wadhifa wa rais katika kinyang'anyiro kikali ambapo wagombea hao wanakwenda takriban sambamba.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoniuliofanyika baada ya mashambulio ya kigaidi mgombea wa chama cha mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen amezidi kusonga mbele ya mgombea anayewakilisha siasa za mrengo wa kati Emmanuel Macron.

Frankreich Emmanuel Macron
Mgombea wa mrengo wa kati Emmanuel MacronPicha: Getty Images/AFP/M. Bureau

Wakati hapo awali Macron alionekana kuwa na uwezekano wa kushinda katika duru ya kwanza kwa asilimia 24.5 ya kura  sasa amerudi nyuma kwa nusu pointi, wakati Marine Le Pen amepanda juu kwa pointi moja zaidi na kufikia asilimia 23.

Mgombea mwengine mkuu anayewakilisha siasa za kihafidhina Francois Fillon aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Ufaransa pamoja na mgombea kutoka siasa za mrengo wa shoto Jean-Luc Melanchon pia wamerudi nyuma kwa nusu pointi.  Mashambulio ya kigaidi yaliyotokea katikati ya mji mkuu, Paris yamekifanya kinyang'anyiro cha leo kisiweze  kutabirika.

Rais wa Marekani  Donald Trump ameliambia shirika la habari la AFP kwamba huenda mashambulio hayo yakamuongezea kura kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen. Trump amesema Le Pen ni mwanasiasa imara juu ya swala la ulinzi wa mipaka ya Ufaransa.  Hata hivyo rais huyo wa Marekani ameeleza kwamba hamuungi mkono Le Pen waziwazi kabisa.

Kura za maoni zinaonyesha kwamba uchaguzi wa Ufaransa umezidi kuwa mgumu kutokana na wagombea wengine kuendelea kulipunguza pengo baina yao na wagombea wanaoongoza katika kura za maoni ,Emmanuel Macron na Marine Le Pen.  Macron alithibitisha uwezo wa kutoa hoja zilizokuwa na nguvu wakati wa mjadala wa televisheni uliofanyika tarehe 20 ya mwezi uliopita.

Hali ya wasiwasi.

Uchaguzi unaendelea katika hali ya wasiwasi juu ya usalama baada ya mashambulio yaliyotokea Alhamisi iliyopita. Mshambuliaji aliyekuwa na bunduki alimpiga risasi na kumuua polisi mmoja na kuwajeruhi wengine wawili.

Baada ya kikao cha dharura cha baraza la mawaziri waziri mkuu wa Ufaransa Bernard Cazeneuve alitangaza kwamba polisi alfu 50 na wanajeshi watalinda usalama wakati wa uchaguzi.  Waziri mkuu Cazeneuve amesema Ufaransa haitaruhusu maadili yake ya kidemokrasia yavurugwe.  Ulinzi umeimarishwa kwenye vituo vya kupigia kura nchini Ufaransa kote ambapo watu milioni 47 wanawapigia kura wagombea jumla ya 11.  Raia wa Ufaransa wanaoishi nje na wale wa majimbo ya nje walishapiga kura hapo jana.  Matokeo ya awali yanatarajiwa  baada ya vituo vya kupigia kura  kufungwa hapo saa mbili usiku kwa  saa za Ulaya ya Kati.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/AFP

Mhariri: Sudi Mnette