1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito ya kususiwa chama cha FN

23 Machi 2015

Chama cha kihafidhina cha UMP kimekisukuma nafasi ya pili chama cha siasa kali za mrengo wa kulia FN,katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa mikoa nchini Ufaransa

https://p.dw.com/p/1EvTw
Rais wa Zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ambae chama chake cha kihafidhina cha UMP kinaongoza matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa mikoaPicha: Dominique Faget/AFP/Getty Images

Chama cha upinzani cha kihafidhina UMP kikishirikana na waliberali wameibuka na ushindi wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa mikoa nchini Ufaransa,wakikipiga kumbo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,Front National-FN,kilichokuwa kikipigiwa upatu kuwa nguvu ya kwanza ya kisiasa nchini humo.Sura hii mpya imejitokeza kukisalia miaka miwili tu kabla ya uchaguzi wa rais .

Chama cha Kisoshialisti kilichoko madarakani nchini Ufaransa na washirika wake wa mrengo wa kushoto wamepata pigo la nne baada ya lile la chaguzi za mabaraza ya miji,uchaguzi wa bunge la Ulaya na ule wa maseneta mwaka 2014.Hata hivyo kwa mtazamo jumla, wamefanya vyema kuliko ilivyokadiriwa na kujikingia kwa pamoja asili mia 28.24 za kura.

Chama cha kihafidhina cha UMP kinachoongozwa na rais wa zamani Nicolas Sarkozy na washirika wake wa kiliberali wamejikingia asili mia 32.5

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Front National,kilichokadiriwa na taasisi za utafiti wa maoni ya umma kingenyakua si chini ya asili mia 30 ya kura,kimejipatia asili mia 25.75.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya ndani,wagombea 220 wa mrengo wa kulia,56 wa mrengo wa kushito 8 wa FN na 6 kutoka vyama vyenginevyo,wamechaguliwa moja kwa moja katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi.

Duru ya pili itafanyika jumapili Marchi 29 ijayo.Kila upande miongoni mwa vyama asilia vya kidemokrasia vya Ufaransa umepania kuwafungia njia wagombea wa chama cha siasa kali FN.

Chama cha Front National kipigwe kumbo duru ya pili

Waziri mkuu Manuel Valls amewatolea wito wafuasi wote wa vyama vya kidemokrasia,wawazuwie wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wasipite duru ya pili."Vipigieni kura vyama vya mrengo wa kushoto au kulia ikiwa katika duru ya pili,wagombea wao watashindana na FN."Amesema.

Frankreich Paris Departementswahlen Marine Le Pen
KIongozi wa chama cha siasa kalai za mrengo wa kulia Marine Le PenPicha: Reuters/G. Fuentes

Wito kama huo wa kukisusia chama cha siasa kali za mrengo wa kulia umetolewa pia na mwenyekiti wa UMP,rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.

Asili mia 50 tu ya wapiga kura ndio walioteremka vituoni jana.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman