Wafuasi wa Sadr waondoka majengo ya serikali
30 Agosti 2022"Bado naamini kwamba wafuasi wangu ni watu wenye nidhamu na watiifu. Na ikiwa ndani ya dakika sitini kutoka sasa hawakuondoka kwenye eneo hilo pamoja na kwenye bunge, basi nitawaacha mkono moja kwa moja." Alisema Muqtada al-Sadr kwa njia ya televisheni akiwalenga moja kwa moja maelfu ya wafuasi wake waliojazana kwenye majengo kadhaa ya serikali katika eneo la Al-Minṭaqah al-Khadhraa, ama Ukanda wa Kijani, wakipambana na vyombo vya usalama vinavyotaka kuwachawanya.
Muda mfupi baada ya kauli yake hiyo ya mchana wa Jumanne (30 Agosti), vyombo vya habari viliripoti kwamba wafuasi hao walianza kuondoka kama walivyoamriwa na kiongozi wao huyo mwenye ushawishi mkubwa.
Umma mkubwa ulikuwa umekusanyika tangu usiku wa Jumatatu (29 Agosti) nje ya eneo hilo, ambalo lina majengo kadhaa ya serikali na ofisi za kibalozi, na sehemu ya wafuasi hao kuingia ndani kabisa ya majengo, wakipambana na vyombo vya usalama.
Kwenye hotuba yake hiyo, Al-Sadr, ambaye siku mbili nyuma alitangaza kujiuzulu kabisa majukumu yote ya kisiasa, aliomba radhi kwa umma wa Wairaq, aliosema kuwa ndio unaobeba machungu ya matukio haya, na wakati huo huo kuwakosowa wale walioyageuza maandamano ya umma kuwa machafuko na mauaji.
"Taifa langu, baada ya kuwa kifungoni kwa ufisadi, kwa masikitiko makubwa sasa limekuwa mfungwa wa ufisadi na ghasia. Nilikuwa nimetegemea maandamano ya amani, ya watu wenye nyoyo safi zilizojaa mapenzi kwa nchi yao, sio wanaokimbilia kutumia bunduki. Hili limeyapotosha mapinduzi haya na sasa mapinduzi haya yanafanana na machafuko na mauaji, sio tena mapinduzi. Na kumwaga damu ya Muiraq yeyote yule ni haramu, haramu, haramu kabisa." Alisema.
Mpasuko wa kisiasa
Mapigano yalianza jana Jumatatu pale vikosi vya usalama viliporusha gesi ya machozi na risasi za moto ili kuwaondosha wafuasi wa al-Sadr kutoka kwenye kasri ya serikali, yenye ofisi ya waziri mkuu, masaa kadhaa baada ya kuivamia.
Hadi sasa, idadi ya watu waliouawa kwenye ghasia hizo imefikia 25 huku wengine 450 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa mashahidi, vyombo vya usalama na vyanzo kutoka wizara ya afya. Wengi katika hao ni wafuasi wa Al-Sadr.
Kauli ya hapo juzi ya al-Sadr kwamba anaachana na siasa, huku kukiwa na mkwamo wa miezi kumi baada ya uchaguzi wa Oktoba kukipa chama chake ushindi mkubwa wa viti bungeni, inatajwa kuifanya hali kuzidi kuwa tete.