Wafungwa watumia mtandao kuwasiliana na wasomaji nje ya jela nchini Zambia.
30 Julai 2007Haijawahi kuonekana kuwa hukumu ya kifo ina nguvu yoyote maalum ya kupunguza uhalifu ama ghasia za kisiasa , kila mahali uzoefu unaonyesha kuwa hukumu hiyo inawatendea ukatili wale wanaohusika katika hatua hiyo. Inatumiwa na kuonyesha ukatili na pia inatumiwa bila kiasi dhidi ya watu masikini.
Benjamin Mawaya baadaye anahitimisha haraka kwa swali kwa kila mtu anayetaka kulijadili suala hili. Iwapo mfumo wa sheria leo hii hauzuwii kutiwa moto kwa nyumba ya mtu aliyefanya kitendo cha kuchoma nyumba nyingine, kubakwa kwa mtu aliyebaka, au kuteswa kwa mtu aliyetesa, sio kwa sababu jamii inaridhia uhalifu huo. Badala yake , ni kwasababu jamii inatambua kuwa inapaswa kujenga mfumo mwingine wa maadili mbali na ule wanaoukataa. Kwa nini tusitumie misingi hii kwa ajili ya hukumu hii ya kifo?.
Uwanja huu wa internet unaomruhusu Mawaya kuelezea wasomaji wake nje ya jela alimofungwa, umetolewa na jumuiya ya Canada inayopambana na dhidi ya adhabu ya kifo, likiwa hili ni shirika la hisani.
Tunatayarisha tovuti kwa ajili ya wafungwa waliohukumiwa kifo duniani kote, amesema mkurugenzi wake Tracy Lamourie.
Wafungwa wanaosubiri hukumu ya kifo nchini Zambia , ambao hivi sasa wanafikia 304 ni wa kwanza katika bara la Afrika kutumia nafasi hii ili kutoa majonzi yao, wakitafuta msaada wa kiroho na fedha , na kupata marafiki nje ya kuta za jela yao.
Ni vipi waliweza kupata kujua juu ya tovuti hizi , Lamourie hafahamu kwa hakika. Lakini njia mojawapo ni kwamba tovuti hizo zimeweza kufahamika kutokana na kupashana habari katika masomo ya biblia katika internet ambayo yanaendeshwa na makanisa nchini Uingereza.
Hivi sasa kila wiki tunapata maombi zaidi na zaidi. Mfungwa mmoja atawaambia wenzake, kuwa watu hawa wamenisaidia kupata marafiki na mahusiano mapya duniani kote, amesema Lamourie.
Mawaya ambaye anangojea rufaa dhidi ya hukumu yake ya kifo kusikilizwa , anaeleza machache kuhusu yeye binafsi katika tovuti yake. Lengo lake la kwanza ni kubadilishana mawazo juu ya hukumu ya kifo, kuuwawa, mateso na Ukristo.
Job Kasonda Kapita, afisa wa zamani wa jeshi la polisi, anamwelezea kila mtu anayetaka kuwa rafiki wake wa kalamu kwanini alihukumiwa kifo mwaka 1994. Nilimpiga risasi na kumuua mtuhumiwa ambaye alionekana kutaka kutumia nguvu ambaye alitaka kumkamata kwa kutaka kufanya ghasia katika eneo la kituo cha polisi mita chache kutoka katika ofisi yake.
Akiwa jela amekuwa mwandishi, akichapisha mashairi katika tovuti yake.
Baadhi ya wafungwa wanatumia tovuti zao kupata misaada pamoja na marafiki. Evans Fundula , mwenye umri wa miaka 33 , ni mmoja wao. Kabla ya kuhukumiwa , nilibarikiwa kuoa na kupata watoto wawili, miaka 14 na 11, wote wasichana . Mke wake alimwacha baada ya kusikia kuwa amehukumiwa kifo na familia yake inahitaji msaada kuwaangalia watoto wake.
Pia anazungumzia kutotendewa haki kwa kutokuwa na fedha za kuweka wakili wa kumtetea. Nyie ni daraja kwetu sisi watu tusiokuwa na uwezo tulio katika sehemu hii ya giza na mbaya.
Haionekani kuwapo na uwezekano wa wafungwa hao kupitishiwa hukumu hiyo ya kifo hasa katika wakati wa utawala wa rais Levy Mwanawasa . Ameahidi kutotia saini utekelezaji wa hukumu za kifo , na pia ameonyesha kuwa hivi karibuni atabadilisha hukumu zote za kifo kuwa kifungo cha maisha. Lakini hadi kutakapokuwa na mabadiliko katika katiba , mahakama zitaendelea kuwahukumu watu kifo, na tovuti za watu waliohukumiwa kifo zitaongezeka katika mtandao wa internet.